Saturday, 28 November 2015

Mtikisiko vigogo TRA hawa tena wasimamishwa kazi


RAIS John Magufuli amemsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade, muda mfupi baada ya ziara ya kushitukiza ya Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa iliyofanyika jana.
Taarifa ya jana ya Ikulu iliyomnukuu Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, imeeleza kuwa hatua hiyo ya Dk Magufuli imechukuliwa baada ya kubaini kupitishwa kwa makontena zaidi ya 300 bandarini bila kulipa kodi na kusababishia hasara Serikali ya zaidi ya Sh bilioni 80. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baada ya kusimamishwa kazi kwa Bade, Rais Magufuli amemteua Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dk Philip Mpango, kukaimu nafasi hiyo mpaka hapo uchunguzi utakapokamilika.
Aidha maofisa wote wa TRA kwa maelezo ya taarifa hiyo, wametakiwa na Rais kutosafiri nje ya nchi, mpaka pale uchunguzi dhidi yao utakapokamilika. Ziara ya Majaliwa Awali jana mchana, Waziri Mkuu Majaliwa akiwa katika ziara hiyo ya kushitukiza, aliwasimamisha kazi maofisa watano na watumishi watatu wa TRA, kutokana na upotevu wa makontena 349 yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 80.
Majaliwa alichukua uamuzi huo baada ya kuzungumza na viongozi wa Mamlaka ya Bandari (TPA) pamoja na wa TRA, ambapo pia alimtaka Bade na Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Lusekelo Mwaseba, washirikiane na polisi kufuatilia upotevu huo na kuhakikisha fedha hizo zinapatikana na kurudishwa serikalini.
Kutiwa jela, kukaguliwa Akitangaza uamuzi huo baada ya kufanya kikao na baadhi ya viongozi wa Serikali bandarini hapo, Waziri Mkuu aliwataja maofisa waliosimamishwa kazi kuwa ni Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki na Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Habibu Mponezya.
“Hawa wanasimamishwa kazi. IGP ninaagiza hawa watu wakamatwe na kuisaidia Polisi. Hati zao za kusafiria zikamatwe na mali zao zikaguliwe kama zinaendana na utumishi wa umma,” alisema Waziri Mkuu.
Maofisa wengine waliosimamishwa kazi ni Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Haruni Mpande, Hamisi Ali Omari (hakutaja ni wa idara gani) na Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu (ICD In-Charge), Eliachi Mrema.
“Hawa wanasimamishwa kazi hadi uchunguzi utakapokamilika na pia wawe mikononi mwa Polisi,” alisema. Pia aliagiza watumishi watatu wa mamlaka hiyo wahamishwe kutoka Dar es Salaam na kupelekwa mikoani, ambao ni Anangisye Mtafya, Nsajigwa Mwandengele na Robert Nyoni.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemwagiza Katibu Mkuu wa Hazina, Dk Servacius Likwelile ambaye alikuwepo kwenye kikao hicho, kuhakikisha anapeleka wataalamu kutoka Wakala wa Serikali Mtandao (e-Govt) haraka iwezekanavyo, ili wakakague mifumo ya taarifa na kubaini jinsi ambavyo wizi huo unafanyika.
“Ninataka uchunguzi uanze kufanyika mara moja, tafuteni njia ambazo zinatumika kama mianya ya wizi kutokea hapa bandarini hadi kwenye ICDs. “Nataka hayo makontena yatafutwe hadi yajulikane yako wapi na fedha hiyo ihakikishwe inarudi serikalini,” alisema.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Ernest Mangu, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk Florens Turuka, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, Mkurugenzi wa TPA, Awadh Massawe na viongozi mbalimbali kutoka TRA na TPA.
‘Kujikanyaga’ kwa Bade Mapema akijibu maswali ya Waziri Mkuu, Kamishna Mkuu wa TRA, Bade alikiri kwamba kuna upotevu wa makontena ambao huwa unafanyika kati ya bandarini na ICDs na hasa ICD ya Ubungo.
Akitoa ufafanuzi, alisema kwamba walifanya ukaguzi kwenye ICD moja na kukuta makontena 54 yamepotea kwa njia za wizi. “Hata hivyo, tulipoendelea na ukaguzi, namba iliongezeka na kufikia 327. Tunaendelea kufuatilia kwa kushirikiana na Takukuru (Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa).
Mmiliki wa ICD ametakiwa kulipa faini Sh bilioni 12.6 na ameshalipa Sh bilioni 2.4,” alifafanua. Alipoulizwa na Waziri Mkuu kama ana majina ya watumishi wanaohusika na wizi huo, Bade akakiri kwamba anayo lakini siyo kwa wakati huo labda ayapate kutoka kwa wasaidizi wake.
Ndipo Waziri Mkuu akamuonesha orodha ya makontena 349, ambayo ni mengi kuliko aliyosema Bade, yenye taarifa zote hadi namba za magari yaliyobeba mizigo hiyo, ambapo Kamishna huyo Mkuu wa TRA, akakiri kwamba orodha hiyo ni ya kweli. “Kwa utaratibu huo hatuwezi kufika, labda baadhi ya watu waondolewe kazini,” alisema Waziri Mkuu na kuanza kutaja majina ya maofisa hao waliosimamishwa kazi.

No comments:

Post a Comment