Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Abdallah Bulembo alisema kuwa Jumuiya ya Wazazi inapongeza maelekezo mbalimbali ambayo yametolewa na Rais Magufuli ambayo yanajenga msingi bora wa mafanikio.
“Chama kimepata kiongozi bora lakini pia nchi imepata Rais bora na hili linaendelea kujidhihirisha katika mambo ambayo yameanza kufanywa na Rais wetu na pia katika maelekezo yake kwa viongozi wa chini, sisi umoja wa wazazi tunapongeza sana kwa hayo,” alisema Bulembo.
Bulembo alisema amefanikiwa kuwa karibu na Rais Magufuli katika kipindi chote cha kampeni kitu ambacho amekiona ni kuwa Rais ni mtu anayesimamia wakati wote na kauli zake.
“Muda tuliokuwa na Rais katika kipindi cha kampeni tumejifunza kitu kwake, huyu ni mtu ambaye akisema jambo ndilo hilo hilo na analisimamia watu wasiwe na hofu naye hana nguvu ya soda,” alisema Bulembo.
Baadhi ya mambo ambayo yamefanywa na Rais Magufuli ni pamoja na kufanya ziara ya ghafla katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kutoa maelekezo ya kuboresha huduma katika hospitali hiyo ikiwa ni pamoja na kufanyiwa matengenezo kwa kipimo cha MRI, ziara ya ghafla Wizara ya Fedha, kufutwa kwa sherehe za Uhuru Desemba 9 mwaka huu na pia Siku ya Ukimwi, Desemba Mosi.

No comments:
Post a Comment