Mbunge mteule wa Jimbo la Mbeya Vijijini kupitia Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Oran Njeza, ameahidi kutekeleza ahadi zote alizozitoa wakati wa
kampeni zikiwamo zilizitolewa na wagombea udiwani kupitia chama hicho
walioshindwa.
Njeza alitoa ahadi hizo juzi akiwa katika mji mdogo wa Mbalizi, muda
mfupi baada ya kukabidhiwa hati ya ushindi na kuwaonyesha wapiga kura
wake.
Aliwataka wananchi kumpa ushirikiano wakati atakapoanza kutekeleza ahadi
hizo, huku akidai kuwa atahakikisha kila kilichoahidiwa na mgombea
udiwani wa CCM ambaye hakushinda pia kinatekelezwa.
“Kuna baadhi ya wagombea wa nafasi za udiwani kupitia chama chetu katika
kata mbalimbali za jimbo hili ambao kura hazikutosha, lakini natambua
kuwa waliahidi vitu vingi vizuri kwa ajili ya maendeleo ya jimbo letu,
nawaahidi kuwa nitazitekeleza zote hata kwa kutumia rasilimali zangu
binafsi” alisema Njeza.
Alisema yeye atafanya kazi bila kuwabagua wananchi wa jimbo hilo kwa
namna yoyote ile huku akiwataka madiwani wote walioshinda kupitia vyama
vingine vya siasa kushirikiana naye katika shughuli za maendeleo ya
jimbo hilo bila kujali itikadi za vyama vyao.
Aliongeza kuwa atahakikisha katika miaka yote atakayofanya kazi kama
mbunge, watu wa Mbeya vijijini wanabadili maisha yao kwa kuboresha
huduma za jamii ikiwamo huduma za afya na maji.
Aidha, alisema kuwa atahakikisha wananchi wa jimbo hilo wanapatiwa
pembejeo za kilimo ikiwamo mbolea ya ruzuku kwa wakati ili waweze
kuboresha kilimo na kuwa na uhakika wa chakula na ziada kwa ajili ya
biashara.
Alisema ushuru na michango isiyokuwa ya lazima atahakikisha inaondolewa
ili watu wafanye maendeleo mengine ya familia zao kutokana na mapato
wanayopata kwenye kilimo na biashara ndogo ndogo wanazofanya.
Njeza aliwataka wananchi kuanza maandalizi ya kuunda vikundi kwa ajili
ya kupatiwa mikopo iliyoainishwa kwenye Ilani ya CCM inayoelekeza kuwa
kila kijiji kitapatiwa Sh. milioni 50, kwa ajili ya wanawake na vijana,
ili iwe rahisi kuzipata kwa kukopeshwa punde fedha hizo zitakapoanza
kutolewa.
Katika hatua nyingine mbunge huyo aliwataka wananchi kuacha kufanya
mambo ambayo yanaweza kusababisha uhasama miongoni mwao, huku akiahidi
kujenga upya misingi ya CCM aliyodai kuwa imebomolewa na watu
anaowatuhumu kuwa ni wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), katika kata ya Nsalala wakati wanashangilia ushindi wa diwani
wa chama chao.
No comments:
Post a Comment