Siku
chache baada ya vyombo vya habari kuripoti mjamzito kujifungulia
kwenye korido ya Kituo cha Afya Lyabukande, Shinyanga kwa kukosa huduma,
uongozi wa Halmashauri ya Shinyanga umewasimamisha kazi watumishi
wawili wa kituo hicho kwa tuhuma za uzembe.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Kiomoni Kibamba ambaye kwa sasa
ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, jana aliwataja
waliosimamishwa kuwa ni pamoja na muuguzi msaidizi wa kituo hicho, Zulfa
Mussa na mhudumu katika maabara, Peter Mazengo.
Kibamba
alisema wamewasimamisha kazi na kufunguliwa mashtaka ya kukiuka maadili
ya utumishi huku wakipewa siku 14 kujibu kwa utaratibu wa ajira ya
utumishi.
“Baada ya hapo tunasubiri baraza la madiwani ndilo litatoa uamuzi juu yao.”
Alisema
wakati tukio hilo linatokea, watumishi hao walikuwa zamu na kushindwa
kumsaidia mjamzito huyo na kitendo hicho kilibainika kuwa cha makusudi
na uzembe wa wazi.
“Awamu
hii ya tano ni awamu nyepesi kwa kufanya kazi sababu imenyooka na iko
wazi. Mtu anayeona hawezi kwenda na kasi atupishe ili wabaki wanaoweza
kutekeleza majukumu yao kwa kufuata kanuni, taratibu na sheria za nchi
na nilishasema mara kwa mara suala hili,” alisema Kibamba.
Kamati
iliyoteuliwa kuchunguza jambo hilo, ikiongozwa na Mganga Mkuu wa Wilaya
ya Shinyanga, Dk Athuman Pembe ilibaini kuwa baada ya mjamzito huyo
kujifungua kwenye korido, watumishi ambao hawakuwapo bali walipata
taarifa na kufika kumhudumia mtoto ambaye ana afya nzuri na baada ya
muda aliruhusiwa kurudi nyumbani.
Ilivyotokea
Tukio
la mjamzito huo, Margareth Charles (22), mkazi wa Kijiji cha Kizungungu
lilitokea Julai 2 baada ya kuelezwa na mtaalamu wa maabara kuwa hakuna
huduma waende sehemu nyingine, lakini mama huyo alishindwa kutokana na
uchungu.
Mtendaji
wa Kata ya Lyabukande, Julius Lugende alisema wananchi wamekuwa
wakikilalamikia kituo hicho kwa muda mrefu na ilifikia wakati
waliandamana kuwakataa watumishi waliopo kutokana na wajawazito
kunyanyasika na kujifungua bila usaidizi.
No comments:
Post a Comment