Licha ya
lori lililokosa breki katika Mlima Iwambi nje kidogo ya Jiji la Mbeya,
kuyakwepa magari manne, limeyagonga mengine manne na kusababisha vifo
vya watu wanne na majeruhi 22.
Ajali hiyo ilitokea juzi usiku katika mji
mdogo wa Mbalizi, Barabara Kuu ya Mbeya - Tunduma, ambako lori hilo
liligonga basi aina ya Toyota Coaster na magari madogo matatu.
Katika
tukio hilo, watu watatu walifariki muda mfupi baada ya kufikishwa
Hospitali Teule ya Ifisi na hadi tunakwenda mitamboni walikuwa
hawajatambuliwa, huku mwingine aliyetambuliwa kwa jina Philip Cheyo (39)
akifariki jana asubuhi katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.
Muuguzi Mkuu
wa Hospitali ya Ifisi, Elimate Sanga alisema walipokea miili ya watu
watatu na majeruhi 22 wakiwamo sita waliohamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kutokana na hali zao kuwa mbaya. Sanga alisema
hadi jana asubuhi, ali- kuwa na wagonjwa 12 waliolazwa.
Ofisa Muuguzi
Msaidizi wa Hospitali ya Rufaa, Lucy Elias alisema Cheyo ambaye alikuwa
mmoja wa majeruhi sita, alifariki jana asubuhi akiwa chumba cha wagonjwa
wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya,
Dhahiri Kidavashari alisema wanachunguza chanzo cha ajali hiyo ingawa
taarifa za awali zinaonyesha kuwa lori lilifeli breki wakati likiteremka
mlima huo.
Akisimulia tukio hilo, kondakta wa lori hilo, Wilberd Joseph
akiwa wodi ya nne ya Ifisi alisema lilianza kuongeza mwendo wakati
wakianza kuteremka mlima huo na ndipo dereva akalalamika halina breki.
“Nilisikia dereva ananiambia, tuombe Mungu, breki zimegoma kabisa, ndipo
lori likazidi kuchanganya na dereva alijitahidi kuyakwepa magari zaidi
ya manne hivi, lakini tulipoingia mjini kabisa (Mbalizi), kulikuwa na
(basi dogo) Hiace ikitokea upande wa kushoto kuingia barabara kuu,
alipolikwepa tela likagonga basi jingine aina ya Coaster lililokuwa
limesimama upande wa kulia,” alisema kondakta huyo.
Alisema baada ya
kugonga basi hilo lililokuwa likitokea Tunduma kwenda Mbeya, pia
liligonga magari mengine yaliyokuwa nyuma ya Coaster hiyo.
Mmoja wa
majeruhi wa basi hilo, Isack Mwaipaja aliyelazwa katika Hospitali ya
Ifisi, alisema walipofika Mbalizi dereva wao hakutaka kuingia stendi na
aliamua kuteremsha abiria pembeni mwa barabara kuu ndipo ghafla
wakasikia kishindo.
No comments:
Post a Comment