MECHI maalum ya kuenzi mchango wa Wayne Rooney na pia kuanzisha Mfuko maalum wa kusaidia Watoto wenye mazingira magumu imekamilika kupangwa.
Mechi hii itachezwa Old Trafford Jumatano Agosti 3 kuanzia Saa 4 Usiku, Saa za Bongo, kati ya Manchester United na Everton.
Mechi hii, kati ya Klabu pekee ambazo Rooney amewahi kuzichezea, ina lengo la kukusanya Pauni Milioni 5 ili kusaidia Watoto wenye mazingira magumu.
Mechi hii pia itasaidia Mashabiki kukiona Kikosi kipya cha Man United chini ya Meneja mpya Jose Mourinho na itakuwa ni Mechi ya kwanza ya kabla Msimu mpya kuanza kuchezwa Old Trafford kwa karibu Miaka Miwili.
Pia, kwenye Mechi hiyo, FA CUP, ambalo Man United walilitwaa kwa mara ya 12 ikiwa ni Rekodi wanayoshikilia pamoja na Arsenal, litaanikwa Uwanjani ili Mashabiki walione.
Akimmwagia sifa Rooney, Mourinho ameeleza: “Wayne ndie na amekuwa Mchezaji bora wa England kwa zaidi ya Miaka 10 na Mechi hii inastahili kabisa kuenzi yote aliyofanikisha. Naingojea kwa hamu kwani utakuwa Usiku spesho kwetu sote Wawili. Nina hakika Mashabiki wataufanya Usiku huu uwe wa kukumbukwa na kumsaidia Wayne kukusanya Fedha nyingi kuwasaidia Watoto wenye hali ya taabu.”
Mapato yote kutokana na Mechi hiyo, ambayo pia ni kusheherekea Miaka 12 tangu Rooney aihame Everton na kutua Man United, yatagwanywa kupitia Taasisi mpya ya Mfuko wa Rooney uitwao Wayne Rooney Foundation kwenda kwa Vyombo vya Misaada Vinne vilivyotajwa kuwa ni NSPCC, Claire House Children's Hospice, Alder Hey Children's Hospital na Manchester United Foundation.
Akitangaza kuanzishwa kwa Wayne Rooney Foundation, Rooney ameeleza: “Kwangu mimi, hakuna Mechi spesho kama si Man United na Everton. Hizi ndio Klabu pekee nilizochezea kama Mchezaji wa Kulipwa. Nina furaha kutamka sasa kuwa sitachezea Klabu nyingine yeyote.”
Aliongeza: “Nina deni kubwa kwa United na Everton kwa kunipa fursa Kisoka. Kupitia Wayne Rooney Foundation ninataka kurudisha fadhila hizo na wakati huo huo nasema asante sana kwa Klabu hizi kubwa kwa kusaidia maisha yangu ya Soka.”
“Everton na Man United, pamoja na Familia yangu, walinipa sapoti na fursa ya kutimiza malengo na ndoto zangu. Nikiwa na Familia yangu change inanifanya nitambue umuhimu mkubwa wa kila Mtoto kupata fursa ya kukua akizungukwa na mapenzi na sapoti ili wapate nafasi kuonyesha uwezo wao. Natumai Wayne Rooney Foundation na Washirika wake wa Misaada wataboresha na kusaidia Watoto wenye maisha magumu kutokana na kuvunjika Familia zao, kuteswa, ishu za afya au kukosa nafasi za elimu.”
No comments:
Post a Comment