Wednesday, 15 June 2016

Simu Feki Kuzimwa Kesho Rasmi - TCRA

SIMU ziliingizwa nchini zikiwa hazina kiwango kuzimwa rasmi kesho, katika kuhakikisha kila mtu anatumia simu kiwango kwa usalama  na ulinzi wa nchi.

Akizungumza na waandishi habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), Mhandisi James Kilaba amesema kuwa katika uzimaji wa simu wameshatoa elimu juu ya simu hizo.

Kilaba amesema kuwa simu ambazo watu walibadilisha (Flash) nazo zitazimwa kutokana na kufanya hivyo ni kosa la kisheria na mtu anayefanya hivyo kifungo chake ni miaka 10.

Amesema hakuna kitu chochote kinachofanya simu zisiweze kuzimwa hivyo watu wajiandae kwa zoezi hilo na simu zitakazozimwa wametakiwa kuzihifadhi katika mazingira salama.

Aidha amesema wametoa elimu ya kutosha, hivyo kesho kutakuwa na mkutano wa wadau mbalimbali wa makampuni ya simu, na wamiliki wa maduka ya simu pamoja na mafundi katika kubadilishana mawazo wakati wa kuzima simu feki.

‘’Simu feki kesho zitazimwa, hatutakuwa na mabadiliko ya kuongeza muda au vinginevyo kutokana na elimu iliyotolewa juu ya simu ya  feki ambazo baada ya soko kushindikana mjini walipeleka vijijini’’amesema Kilaba  .

No comments:

Post a Comment