England imeshindwa kuongoza Kundi B la michuano ya Euro 2016 baada ya kulazimisha sare ya bila kufungana na Slovakia katika mchezo wa mwisho wa kundi hilo uliochezwa huko Saint-Etiene, Ufaransa.
Hodgson alifanya mabadiliko ya kuwapumzisha wachezaji wake sita wa kikosi cha kwanza, nahodha Wayne Rooney ambaye alikuwa chachu kwenye ushindi dhidi ya Wales pia alianzia benchi kwenye mchezo huo. Lakini kushindwa kupata ushindi dhidi ya Slovakia kunaifanya England kumaliza nafasi ya pili na huenda ikakutana na wakati mgumu kwenye mechi yake ya hatua ya 16 bora.
England walipata nafasi nzuri za kupachika mabao lakini golikipa wa Slovakia Matus Kozacik alikuwa makini kuokoa mchomo wa Jamie Vardy wa kipindi cha kwanza kabla ya kufanya kazi ya ziada kuokoa mpira wa Nathaniel Clyne kipindi cha pili.
Rooney aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Jack Wilshere lakini haikusaidia kubali matokeo mbele ya Slovakia waliozuia kufungwa goli ili kupata pointi moja muhimu kwao.
Shuti la Dele Alli liliokolewa kwenye mstari na Martin Skrtel sekunde chache baada ya kuingia akitokea benchi.
England watasafiri hadi Nice ambako watacheza dhidi ya timu itakayomaliza nafasi ya pili kutoka Kundi F kati ya Hungary, Ureno, Iceland au Austria kwenye mchezo wa 16 bora Jumatatu ijayo.
No comments:
Post a Comment