Tuesday, 24 May 2016

KUELEKEA FAINALI YA UEFA CHAMPIONS LEAGUE: REKODI KALI ZINAZONYATIWA KUVUNJWA KATIKA USIKU WA MILAN

Image result for UEFA

Kuweka rekodi mpya au kuifikia rekodi iliyowahi kuwekwa zamani na kuivunja kabisa ni jambo lenye furaha na fahari kubwa katika nyanja yoyote kimaisha. Lakini endapo kama utafanikiwa kuivunja rekodi hiyo katika mchezo wa fainali wa UEFA Champions League, sio rahisi kuufananisha msisimko wake.
Ndani ya dimba la Giusseppe Meazza (San Sirro) Jumamosi hii kutakuwa na vita ya kuuwania ufalme wa Ulaya baina ya watoto wa mji mmoja, Real Madrid dhidi ya Atletico Madrid umbali wa km 15 za barabara unaweka tofauti ya kimakazi baina ya mahasimu hawa.
Wakati macho na akili za mamilioni ya mashabiki zikielekezwa katika kutaka kujua nani atakayeibuka na ushindi mwishoni mwa kipyenga cha mwamuzi Mark Clattenburg kutoka England, lakini zipo rekodi hizi kali ambazo wataalamu wangu hampaswi kukaa nazo mbali pindi zitakapokuwa katika hatihati ya kutumbuliwa.
  1. Magoli mengi kufungwa na mchezaji mmoja katika fainali ya UEFA Champions
    League
Achana kabisa na mashindano ya hat-trick wanayopeana Ronaldo, Messi na Suarez ndani ya La liga, lakini linapokuja suala la fainali ya UEFA hii ni habari nyingine. Ndiyo maana watatu hawa kwa ujumla wameshacheza mechi 8 tofauti za fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini hakuna aliyewahi tupia kambani mabao mawili ndani ya fainali. Pengine awamu hii mtoto wa Madeira, Christiano Ronaldo, Fernando Torres ‘El Niño’, Gareth Bale na Antoine Griezman (kiboko ya mabishoo Ulaya) wanaweza kuingia katika rekodi ya wakali waliowahi kufunga mabao mawili ndani ya game moja fainali na kujumuika katika orodha hii:
2 goals – Daniele Massaro (AC Milan, 1994), Karl-Heinz Riedle (Borussia Dortmund, 1997), Hernán Crespo (Milan, 2005), Filippo Inzaghi (AC Milan, 2007), Diego Milito
(Internazionale Milan, 2010).
  1. Goli la haraka zaidi mchezo wa fainali UEFA Champions League
Mtaalamu Paolo Maldini ‘El capitano’ ndiye anaishikilia rekodi ya kufunga goli la fasta zaidi. Mnamo sekunde ya 53 tangu mwamuzi Manuel Mejuto González apulize kipyenga cha kuanzisha pambano, tayari AC Milan ilishafanikiwa kupata faulo pembezeni mwa box la Liverpool. Krosi maridadi iliyojazwa na ‘maestro’ Andrea Pirlo iliunganishwa wavuni na captain Maldini na kumfanya golikipa Jerzy Dudek kuianza mechi kwa ‘mkosi’ ndani ya dimba la Atatürk Olympic Stadium, jijini Instabul. Akiwa vilevile ndiye mchezaji aliyewahi cheza mechi nyingi zaidi katika nyasi za San Siro (mechi 902) na kwa heshima aliyopewa ya kulikabidhi kombe uwanjani Jumamosi hii ya fainali, bila shaka Paolo Maldini atakuwa kwenye siti muafaka kabisa na macho katika saa yake ya mkononi kushuhudia kama rekodi yake inaweza vunjwa katika uwanja ‘wake mwenyewe’.
  1. Zidane kuingia katika listi ya wakali waliotwaa taji la Uefa wakiwa wachezaji na baadaye kama makocha
Zinedine Yazid Zidane ‘Zizzou’, ambaye ulimwengu mzima unaamini kuwa mchezaji aliyefunga goli bora zaidi la wakati wote katika michuano ya UEFA, pindi alipopigilia ‘volley’ iliyoipa Real Madrid ushindi wa taji lake la tisa la michuano hii mnamo mwaka 2002. Anayo nafasi ya kuingia katika kumbukumbu ya kihistoria na kuwa mtu wa saba kuwahi twaa taji la Ulaya akiwa ndani ya jezi kama mchezaji na baadaye ndani ya suti ya ukocha.
Wataalamu wengine waliowahi kufanya hivyo ni Miguel Muñoz, Giovanni Trapattoni, Johan Cruyff, Carlo Ancelotti, Frank Rijkaard, na Joseph ‘Pep’ Guardiola.
  1. Cristiano Ronaldo na mbio za kuivunja Rekodi yake ya mabao 17
Akiwa tayari amezifumania nyavu mara 16 katika mechi 11 za UEFA Champions League msimu huu, Ronaldo anahitaji goli moja tu kuifikia rekodi ya mabao 17 aliyoiweka yeye mwenyewe msimu wa 2013/14.
Lakini iwapo atatikisa wavu mara mbili wa golikipa mbishi Jan Oblak, basi rekodi mpya ya magoli 18 ndani ya msimu mmoja itakuwa imewekwa rasmi.
  1. Magoli katika michezo mitatu tofauti ya fainali
Goli moja ndani ya uwanja wa Sansiro litamwezesha Christiano Ronaldo kuwa mchezaji pekee kufunga katika fainali tatu tofauti (2008 akiwa Manchester United dhidi ya Chelsea, 2014 dhidi ya Atletico Madrid).
Unahitaji kuwa na moyo mgumu zaidi ya Farao kama uta-bet dhidi ya CR7 kufumania nyavu katika dakika 90 ama 120 za mchezo huu.
Mashabiki 80,018 ndani ya dimba la Giusseppe Meazza watakuwa wakipaza sauti na kuimba nyimbo za kuvipa sapoti vikosi vyao, wengine tutakuwa tumebanana ndani ya vibandaumiza vyetu pale Keko-Magurumbasi wote tukisubiria kuona rekodi mpya zikisimikwa!Hasta lä Vista!

No comments:

Post a Comment