
Rais John Magufuli analipwa Sh9.5 milioni kwa mwezi. Huo ndiyo
mshahara ambao mkuu wa nchi ameutangaza kwa umma bila ya kutoa ufafanuzi
kama unajumuisha marupurupu mengine kulingana na cheo chake.
Rais
ameamua kuweka hadharani masilahi yake wakati kukiwa na mjadala mkubwa
uliotokana na tamko lake alilolitoa mapema wiki hii kuwa atapunguza
mishahara ya watendaji wakuu wa taasisi na mashirika ya umma kutoka Sh40
milioni hadi Sh15 milioni, akisema katika “Serikali ya Magufuli”,
ambayo itadumu kwa miaka 10 iwapo atachaguliwa tena mwaka 2020, hakuna
mtu atakayelipwa zaidi ya kiwango hicho.
Dk Magufuli, ambaye
hivi sasa yuko nyumbani kwake Chato mkoani Geita kwa mapumziko aliamua
kutangaza mshahara wake baada ya wabunge wawili, Zitto Kabwe (ACT
Wazalendo) na Tundu Lissu (Chadema) kuripotiwa kutaka atangaze mshahara
wake baada ya tamko la kupunguza mishahara ya vigogo wa mashirika hayo
ya umma.
Wakati wa kipindi cha asubuhi cha 360 kinachorushwa na
kituo cha televisheni cha Clouds, watangazaji walisoma habari hiyo na
kuanza kujadili mshahara wa Rais.
Wakati wakijadili ndipo Rais alipowapigia simu kuwatajia mshahara wake.
Meneja
wa kipindi cha 360 ambacho hufanya uchambuzi wa magazeti, Hudson Kamoga
alithibitisha kuwa Rais Magufuli alimpigia simu kumtajia
mshahara wake.
“Aliniuliza kwa nini sikuwapo kwenye kipindi, nikamjibu kuwa nipo Arusha kwa majukumu mengine,” alisema Kamoga.
“Akaniambia
niwaambie wenzangu ambao wapo kwenye kipindi kuwa mshahara wake wa
mwezi ni Sh9.5 milioni na mshahara huo ameukuta na kwamba akirudi Dar es
Salaam, twende ofisini kwake akatuonyeshe salary slip.” Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Gerson Msigwa alisema Ikulu hakuna
mtu anayelipwa zaidi ya Sh9.5 milioni.
“Kwa hiyo kama Rais
ameamua kuzungumza nao (Clouds) kuhusu mshahara wake, naomba asubiriwe
akirudi Dar es Salaam akawaonyeshe salary slip yake kama atafikia hatua
hiyo,” alisema Msigwa. Lakini uamuzi wake wa Rais kutangaza mshahara
wake, umekosolewa na Lissu.
“Mshahara alioutangaza Rais
unaendelea kuwaweka wananchi njiapanda kwa kuwa hauna uchanganuzi,”
alisema Lissu alipoulizwa maoni yake kuhusu kiwango cha mshahara wa mkuu
wa nchi.
“Anapaswa kueleza iwapo ni fedha ya jumla, marupurupu
yapo humo ndani kwa sababu mshahara wa mbunge ni Sh3.6 milioni na
anapohesabiwa marupurupu yake inafikia kiasi cha Sh12 milioni na hizi
ndizo anazoondoka nazo.
“Sasa tunahitaji kujua kama ndiyo fedha anayokwenda nayo nyumbani au ni vinginevyo.”
Kabla
ya Dk Magufuli kufanya hivyo, kumekuwa na mjadala kwa muda mrefu kuhusu
mshahara wa Rais, na kila vyombo vya habari vilipojaribu kutaja, Ikulu
ilikanusha mara moja lakini haikutoa ufafanuzi wa kiwango sahihi cha
mshahara.
Mtandao wa African Review mwaka jana ulifanya
uchambuzi wa mishahara ya marais Afrika na uliwataja marais watano
wanaoongoza kwa kuwa na mishahara mikubwa kwa mwaka kuwa ni Paul Biya wa
Cameroon anayelipwa dola 610,000 za Marekani, akifuatiwa na kiongozi wa
Morocco, Mfalme Mohammed VI (dola 480,000) na Rais Jacob Zuma wa Afrika
Kusini (dola 272,000).
Katika orodha hiyo, Rais mstaafu wa
Tanzania, Jakaya Kikwete alishika nafasi ya nne akitajwa kupata dola
192,000 na wa tano alikuwa Rais Abdel Aziz Bouteflika wa Algeria,
anayelipwa Dola168,000.
Madhumuni ya utafiti wa mtandao huo
yalikuwa ni kuangalia kiasi wanacholipwa marais wa Afrika kwa mwaka na
kile inachopata taifa husika kwa muda huo.
Pia walilenga kuangalia uhusiano wa viongozi na wananchi wa kawaida wanaowangoza.
No comments:
Post a Comment