Polisi mkoani Mwanza, ndugu, jamaa na marafiki, juzi, walilazimika kufukua
kaburi na kutoa mwili wa Gelinde Masumbuko baada ya kuzikwa na ndugu wa
marehemu Said Mussa na kukaa kaburini kwa siku mbili.
Hatua
hiyo ilifikiwa baada ya wahudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti cha
Hospitali ya Mkoa wa Mwanza wa Sekou-Toure, kuukabidhi mwili wa
Masumbuko kwa ndugu wa Mussa.
Baada ya kukabidhiwa mwili huo,
ndugu wa Mussa waliendelea na taratibu na kuuzika katika makaburi ya
Nyashana wilayani Ilemela, kabla ya ndugu wa Masumbuko kubaini kuwa
mwili wa ndugu yao uliokuwa umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia
maiti hauonekani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Justus
Kamugisha alisema walilazimika kuingilia kati suala hilo baada ya ndugu
wa Masumbuko kuripoti tukio la mwili wa ndugu yao kupotea katika
mazingira ya kutatanisha.
“Baada ya uchunguzi kwa kushirikiana
na uongozi wa hospitali tulibaini yalifanyaka makosa kwa mwili huo
kukabidhiwa kwa ndugu wa marehemu Mussa ambao tayari walishauzika,”
alisema.
Uchunguzi huo ulibaini mwili wa Mussa ulikuwa bado umehifadhiwa
katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali hiyo.
“Ilibidi
taratibu za kisheria zichukuliwe na mwili wa marehemu Masumbuko
kufukuliwa na kukabidhiwa kwa ndugu zake, huku ndugu wa Mussa nao
wakichukua mwili wa ndugu yao kwa mazishi mapya,” alisema Kamugisha.
Mkanganyiko
huo ulitokea baada ya ndugu wa Masumbuko kutoka Sengerema kufuata mwili
katika hospitali hiyo na kuukosa, hali iliyowalazimu kufuatilia ili
kujua alikozikwa na taratibu za kuufukua zifuatwe.
Ndugu wa Masumbuko, Finias Elias, alisema walitarajiwa kumzika jana nyumbani kwao wilayani Sengerema.
Ndugu
wa marehemu Mussa, Said Mussa alisema waliotumwa kuuchukua mwili wa
marehemu walishindwa kumtambua kutokana na kuvimba uso.
No comments:
Post a Comment