Monday, 21 March 2016

ULIMWENGU KUUNGANA NA STARS ADDIS ABABA


MSHAMBULIAJI wa TP Mazembe ya DRC, Thomas Ulimwengu ataungana na wachezaji wa Azam FC mjini Addis Ababa, Ethiopia kesho asubuhi kwa safari ya Chad kwenda kuungana na timu ya taifa, Taifa Stars.
Rais wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Ravia Idarus Faina ambaye ndiye mkuu wa msafara wa Taifa Stars, ataondoka Dar es Salaam kesho Jumanne alfajiri na wachezaji walionaki kwenda Chad kwa ajili ya mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2017.
Kundi hilo la pili lenye wachezaji wanane, linatarajiwa kuungana na Ulimwengu kesho asubuhi Addis Ababa kisha kuunganisha safari ya kuelekea nchini Chad wanapotarajiwa kufika saa 6:00 mchana.
Wachezaji wa Azam wanaotarajiwa kusafiri kesho Jumanne alfajiri ni Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, David Mwantika, Himid Mao, Farid Mussa na John Bocco.
Ikumbukwe kundi la kwanza la wachezaji wa Stars liliwasili jana nchini ni Chad. Waliotangulia ni Ally Mustafa 'Barthez', Juma Abdul, Haji Mwinyi, kelvin Yondani, Deus Kaseke, Mohamed Hussein, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Ibrahim Ajibu, Shiza Kichuya, Mohamed Ibrahim na Nahodha Mbwana Samatta.
Wakati Ulimwengu alichelewa kutokana na kuwa anaitumikia klabu yake, Mazembe Jumapili katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya St George ya Ethioppia, wachezaji wa Azam nao walikuwa wana mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini.
Kesho Jumanne wachezaji wote watafanya mazoezi mepesi ya mwisho ya pamoja katika uwanja wa Omnisport Idriss Mahamat Ouya saa 9 mchana, kabla ya kuwavaa wenyeji siku ya Jumatano katika uwanja huo huo.

No comments:

Post a Comment