Tuesday, 29 March 2016

Rais Magufuli Aagiza kufunguliwa kwa barabara ya Uwanja wa Ndege Mwanza -Igombe hadi Kayenze


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa tanzania Dakta John Magufuli, ameagiza kufunguliwa kwa barabara ya Uwanja wa Ndege Mwanza -Igombe hadi Kayenze yenye urefu wa km.7 iliyofungwa kupisha upanuzi wa uwanja huo tangu mwaka 2014 na kusababisha usumbufu kwa wananchi waliokuwa wakiitumia hususan wa wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Rais Dakta Magufuli ametoa kauli hiyo mara baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa Mwanza kabla ya kuelekea nyumbani kwake wilayani Chato mkoani Geita kwa mapumziko wakati akizungumza na viongozi wa serikali wa mkoa wa Mwanza, vyama vya siasa, madhehebu ya dini, wananchi na waandishi wa habari waliokuwepo kumpokea uwanjani hapo.

Dakta. Magufuli amemwambia Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, kuwa anatumia fursa hii kukuagiza kufunguliwa kwa barabara hiyo ambayo anatambua inapita pembezoni mwa uwanja wa Ndege wa Mwanza lakini serikali itaangalia juu ya kuupanua zaidi kuelekea eneo la mashariki ili kutoa nafasi ya barabara kutumiwa na wananchi wa maeneo haya.

 "Nafahamu suala linalowaumiza wananchi la kufungwa kwa barabara ya Airpot-Igombe  yenye urefu wa km7, sasa naagiza kuanzia sasa  kufunguliwa kwa barabara hiyo ili wananchi watumie kupita ili kuondoa usumbufu wa kuzunguka kule maeneo ya Nyakato hadi maeneo ya TX Kata ya Bugogwa, Kata ya Sangabuye,”alsema.

Dakta magufuli amesema serikali katika bajeti ya mwaka 2016/2017 imepanga kutoa fedha kwa lengo la kuhakikisha ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza unaoboreshwa kuwa wa kisasa ili kuwezesha ndege kubwa kutua kwa wingi lakini pia kutumiwa kimataifa na nchi za Maziwa Makuu kama alivyoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2015.

Aidha amesisitiza kwa kusema kuwa “kamwe sitaki kusikia tena uwanja huu umefungwa na uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA) kuangalia kuupanua zaidi kwenda mashariki ili barabara hii pia waitumie wananchi na tutatoa fedha ili ijengwe kwa kiwango cha lami hata kama ni kwa awamu,”

Baada ya kuzungumza na baadhi ya viongozi wa mkoa wa Mwanza, ghafla Rais Dakta Magufuli alitoka nje na kuelekea eneo la mighahawa iliyopo nje ya uwanja wa ndege wa Mwanza na kuingia katika moja ya mghahawa na kusalimiana na wateja na wananchi waliokuwa katika maeneo hayo kisha kuagiza chakula na kula pamoja na kuagiza kupewa vinywaji baridi kwa wananchi waliokuwepo eneo hilo.

Kutokana na tukio hilo baadhi ya wananchi waliokuwepo katika eneo hilola mgahawa ambao alikuwa anapata chakula na baadhi ya viongozi wakiwemo madhehebu ya dini na serikali, wameeleza kufurahishwa kwao na hatua hiyo huku mmiliki wa mgahawa huo  akiahidi kubadilisha jina la mghahwa wake na kuupatia jina la Dk Magufuli Cafe ili kuenzi kufika kwake na kula chakula hapo ukizingatia kuwa ni kiongozi mkubwa wanachi.

Huku viongozi wa madhebu ya dini wakiendelea kumuombea sala na dua ili kuendelea kuwatumikia watanzania bila kuchoka na kuhakikisha amani na umoja wa taifa unaendelea kuwa tunu, lakini pia katika dua na sala zao wamemuhakikishia Rais Dk Magufuli kuendelea kumuombea na kumpatia ushirikiano wao ili aweze kutekeleza majukumu yake akiwa na nguvu na afya njema.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida mara baada ya kusalimiana na viongozi mbalimbali waliofika kumpokea alipowasili majira ya saa uwanjani hapo majira ya asubuhi ghafla Rais magufuli alikwenda eneo walipokuwa wamesimama watumishi wa uwanja huo na kuwasalimia kwa kushikana nao mikono.

Nao abiria waliokuwa wakisubiri kusafiri na ndege kuelekea jijini Dar es salaam na Bukoba na kwingineko walifurahi kumuona Rais Dk Magufuli na kuchangamkia kusalimiana nae kwa kushikana naye mikono na kuonyesha furaha kwa kitendo hicho cha kumuona kiongozi wao huku baadhi wakidai ni jambo lisilo la kawaida.

Rais Dk Magufuli aliwapongeza kwa sala na dua viongozi wa madhehebu kwa kuendelea kumuombea ili kuweza kuwatumikia wananchi bila kuwabagua kwa itikadi zao za kisiasa na kusisitiza kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa kufanya kazi bila kuchoka ili kila mtanzania aweze kunufaika na rasilimali zilizopo nchini kisha kuomba ushirikiano kwa wananchi wote ili kufikia malengo.

Kurugenzi ya Mwasiliano ya Rais, IKULU
Dar es salaam
29 Machi, 2016

No comments:

Post a Comment