WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa anatarajia kuwa mgeni rasmi kwenye
Tamasha la Pasaka linalotarajia kufanyika Machi 28 kwenye uwanja wa
Taifa mjini Kahama.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa
Kamati ya maandalizi ya Tamasha la Pasaka, Alex Msama Profesa Mbarawa
amekubali kuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo ambalo linashirikisha
waimbaji mbalimbali wa nyimbo za Injili.
Msama alisema Profesa Mbarawa
kukubali kuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo ni ishara kwamba tamasha
hilo halijaegemea upande mmoja wa dini kama inavyodhaniwa na baadhi ya
wadau wa muziki huo.
“Tunampongeza Profesa Mbarawa
kuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Pasaka, kwani huwa halijali dini,
jinsia wala kabila katika utekelezaji wake,” alisema Msama.
Msama alisema hivi sasa kamati
yake ya maandalizi inaendelea na mchakato wa kufanikisha tamasha hilo
ambalo litaanzia mkoani Geita Machi 26, Mwanza Machi 27 na kumalizia
Kahama Machi 28.
Msama anataja viingilio katika
tamasha hilo ni shilingi 5000 kwa wakubwa na shilingi 2000 kwa watoto
ambako kupitia tamasha hilo amepanga kugawa baiskeli za walemavu 100 kwa
wakazi wa mikoa hiyo na kwingineko.
Waimbaji waliothibitisha
kushiriki tamasha hilo ni Rose Muhando, Upendo Nkone, Joshua Mlelwa,
Jesica BM, Christopher Mwahangila, Christopher Mwabuka, Jenipher Mgendi,
Bonny Mwaitege, Goodluck Gozbert, Kwaya za Wakorintho Wapili ya Mafinga
na AIC Makongoro Vijana ya jijini Mwanza na wengineo wengi.
No comments:
Post a Comment