Tuesday, 8 March 2016
BOCCO AMEZALIWA KUZIFUNGA YANGA/SIMBA, NI MSHAMBULIZI MKALI ZAIDI AMBAYE HAJATOKEA
Na Baraka Mbolembole
Mechi yake ya kwanza tu kukutana na Yanga SC alifunga bao, na kufikia mechi ya 16 ya ligi kuu Azam FC dhidi ya Yanga, mshambulizi John Bocco tayari amefunga jumla ya magoli 10. Kama Bocco angefunga magoli hayo akiwa mchezaji wa Simba SC bila shaka angetajwa mshambulizi bora kuwahi kutokea nchini lakini bado sifa hiyo haitapotea licha ya kwamba magoli hayo ameifunga Yanga akiwa mchezaji wa Azam.
MISIMU 8 VPL, STAA ZAIDI AZAM FC
Bocco ndiye mchezaji aliyefunga goli lililoipandisha ligi kuu Azam FC mapema mwaka 2008 na klabu hiyo ya Temeke, Dar es Salaam ikacheza msimu wake wa kwanza katika VPL (2008/09) msimu ambao walinusurika kushuka daraja, kama si kuifunga Yanga 3-2 siku ya mwisho wa msimu.
Bocco ni mshindi binafsi wa tuzo ya ufungaji bora wa ligi kuu msimu wa 2011/12 alipofunga magoli 16 na kuiwezesha Azam FC kumaliza katika nafasi ya pili kwa mara ya kwanza. Pia mshambulizi huyo mrefu ndiye mfungaji wa goli lililowahakikishia Azam FC ubingwa wake wa kwanza wa VPL katika msimu wake wa sita tu.
Achana na magoli yake kumi katika VPL, Bocco ameifunga tena Yanga zaidi ya magoli manne nje ya michezo ya VPL. Ni kielelezo tosha cha mfungaji mkali zaidi ambaye mabeki wa Yanga wameshindwa kumzima kwa misimu nane sasa.
MECHI 34, MAGOLI 8 STARS
Bocco aliitwa kwa mara ya kwanza katika timu ya taifa ya (Taifa Stars) kwa mara ya kwanza mwaka 2009 akiwa U20. Mbrazil, Marcio Maximo ndiye kocha wa kwanza kumjumuhisha nahodha huyo wa Azam katika timu ya Taifa na kuanzia wakati huo hadi sasa Bocco amefanikiwa kuichezea Stars mara 34 na kuifungia magoli 8 tu.
Amecheza chini ya Maximo, Wadenish, JAN na KIM Poulsen, M-holland, Martin Nooij na sasa chini ya Mzawa, Charles Boniface Mkwasa. Kwanini hafungi sana akiwa na timu ya Taifa?
Kuna wakati Bocco aliamua kustaafu kuichezea Stars baada ya kukutana na zomeazomea ya mashabiki wa klabu za Yanga na Simba. Ilikuwa mapema mwaka 2011 na ndiyo kwanza alikuwa na miaka 22. Lakini wadau mbalimbali walimshauri mchezaji huyo kubadili uamuzi wake huo, naye akarejea na sasa ni kati ya manahodha wa Stars.
Cha kujiuliza ni kwa nini mchezaji huyo amekuwa si mfungaji sana akiwa katika timu ya taifa. Ameifunga Simba zaidi ya mara kumi, na tayari amefunga zaidi ya magoli 14 dhidi ya Yanga. Kuzifunga Simba na Yanga zaidi ya magoli 25 kwa misimu 8 si jambo dogo.
KLABU INAMTHAMINI, BOCCO ANAITHAMINI AZAM FC
Kumekuwa na uvumilivu wa hali ya juu kutoka upande wa Azam FC dhidi ya Bocco, pia mchezaji ameonyesha kutobabaika na baadhi ya ofa zilizowahi kupelekwa klabuni ili kumuhamisha. Baada ya kushindwa katika majaribio yake ya kwanza nchini Israel mwaka 2011, Bocco amewahi kukataa ofa ya kwenda Morocco (2014) na mwaka uliopita alikataa kwenda Afrika Kusini.
Azam inamlipa vizuri, ina mthamini sana, na mchezaji anahitaji kusimika jina lake katika historia ya klabu. Hata kama hajapata nyakati nzuri sana akiwa na Stars, lakini Bocco ni mfungaji ambaye timu za Yanga na Simba hazitamsahau kamwe.
Wakati mchezaji anayeongoza kufunga magoli katika historia ya klabu hizo kongwe nchini ni yule aliyefunga magoli matano tu, Bocco amevuka mara mbili yao, tena akifanya hivyo kwa kila timu.
Bocco ni kama amezaliwa ili kuzifunga Yanga/Simba, Ni mshambulizi mkali zaidi ambaye hajatokea.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment