Thursday, 25 February 2016

Wagombea urais wa Zanzibar wadai kutishwa

WAKATI vyama vya siasa vilivyothibitisha kushiriki katika uchaguzi wa marudio Machi 20 vikiwa katika maandalizi ya mwisho, baadhi ya wagombea wa nafasi za urais wamelalamika kuanza kupokea vitisho na matusi ya kulaumiwa kwa uamuzi wao wa kushiriki katika uchaguzi huo. Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu, mgombea wa nafasi ya urais kupitia chama cha TADEA, Ali Juma Khatib alisema amekuwa akipokea vitisho kutoka kwa viongozi wa vyama vya siasa ikiwemo CUF wakimshutumu kwa kitendo chake cha kuamua chama chake kushiriki katika uchaguzi wa marudio ulioitishwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ZEC.
Alisema amepokea vitisho hivyo kutoka kwa kiongozi mmoja wa chama cha CUF (jina linahifadhiwa) ambaye alitishia maisha yake huku tukio hilo akiliripoti katika kituo cha Polisi cha Zanzibar.
Aidha aliipongeza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar katika hatua za awali za kuwapatia walinzi ambao wanatoka katika jeshi la Polisi kitengo cha Upelelezi watakaotembea nao wakati wa shughuli za kisiasa, lakini pia aliomba ulinzi kama huo uimarishwe katika maeneo ya nyumba zao.
Kauli ya Khatib iliungwa mkono na mgombea wa nafasi ya urais kwa tiketi ya chama cha AFP, Said Soud ambaye aliomba ulinzi zaidi katika kisiwa cha Pemba katika kipindi hiki hadi kuelekea uchaguzi wa marudio kufuatia kuwepo kwa vitisho vinavyofanywa na wafuasi wa baadhi ya vyama vya siasa ambao hawakufurahi kuona wanashiriki katika uchaguzi wa marudio.

No comments:

Post a Comment