Mwenyekiti wa Mbomipa, Christopher Mademla alisema wanao ushahidi kwamba watu hao sio wenyeji wa kata hiyo ya Pawaga na wamerejea eneo hilo siku chache baada ya kuokolewa kuendesha shughuli za kilimo kinyume cha sheria za hifadhi na wanahatarisha maisha yao.
Mbali na kulima katika eneo hilo ambalo ni makutano ya mito Ruaha Mdogo na Ruaha Mkuu, na ambalo pia ni la mapito ya wanyamapori wanaotoka katika hifadhi za Taifa za Ruaha na Mikumi, pia inaelezwa wanatumia eneo hilo kama maficho ya majangili wa meno ya tembo na wanyamapori wengine.
“Baada ya kupata misaada na maji kupungua katika eneo hilo, baadhi ya waathirika wa mafuriko wameanza kurejea katika eneo hilo la hifadhi la Nyaruu walilovamia kwa mwaka wa tatu sasa na taarifa hii nimeitoa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ili tuweze kushirikiana naye kuwaondoa wavamizi hao,” alisema Mademla.
Hivi karibuni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitembelea katika kijiji cha Kisinga, Pawaga ambako ni moja ya maeneo mawili yenye waathirika wa mafuriko hayo na kujionea ukubwa wa tatizo kabla hajapokea misaada kutoka kwa wasamaria na kufanya mkutano wa hadhara alioutumia kutoa pole kwa waathirika.
Katika mkutano huo wa hadhara, Mademla alipewa na Waziri Mkuu nafasi na ndipo alipoitumia kupinga ombi la baadhi ya watu wanaotaka waathirika wa Nyaruu waruhusiwe kuendelea na kilimo katika eneo hilo.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, hawa waathirika unaoongea nao hapa si wale waliokolewa na helikopta. Hawa ni wa kijiji cha Kisanga ni tofauti na wale wa Nyaruu ambao wameanza kurejea katika eneo hilo la hifadhi, watu hao hawatakiwi kulima, kuishi wala kufanya shughuli yoyote ile katika eneo la hifadhi,” alisema Mademla.
Baada ya kusikia hayo, Waziri Mkuu aliagiza suala hilo lishughulikiwe na serikali.
No comments:
Post a Comment