Wednesday, 24 February 2016

300 kufanyiwa upasuaji wa macho


WATU 300 wanatarajiwa kupata huduma ya upasuaji katika hospitali mpya ya Chuo Kikuu cha Dodoma ya Benjamin Mkapa.
Huduma hiyo ya upasuaji imewezeshwa na hospitali hiyo kwa kushirikiana na wataalamu kutoka vyuo vya UTAH (Moran Eye Centre) na Chuo cha Weil Cornell Medicine vyote vya nchini Marekani. Taarifa kutoka hospitalini hapo zinasema kliniki hiyo imeanza Jumatatu na itamalizika leo.
Alisema hadi juzi walikuwa tayari wamewahudumia watu 100. Huduma hizo zinatolewa bure na wataalamu bingwa hao wakiwa wanatumia vifaa vya kisasa vilivyopo katika hospitali hiyo na vingine vilivyoletwa na madaktari hao.
Imeelezwa kuwa huduma hiyo imewezekana kutokana na mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Chuo Kikuu cha Dodoma na vyuo hivyo na wamebaini kuwa Dodoma wana matatizo makubwa ya macho.
Dk Jeff Pettey wa Chuo Kikuu cha Utah akizungumza katika mahojiano, alisema magonjwa waliyobaini ni pamoja na trakoma, uoni hafifu unaotokana na uzee, kuona karibu, mtoto wa jicho na matatizo yanayotokana na wahusika kugongwa au kujigonga na kitu kichwani.
Alisema pamoja na kuja safari hii wamesema wanafanya mpango wa kuja mkoani hapa mara mbili kwa mwaka.
Aidha alisema wakati wanafanya kazi ya kuhudumia wananchi wa mkoa wa Dodoma na majirani pia wanasaidia kuwafundisha madaktari wa kitanzania kuhusu magonjwa mbalimbali ya macho na upasuaji wake.
Mwalimu wa Chuo cha Afya cha Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Frank Sundai, alisema wanafaidika na huduma hizo ambazo pia zinasaidia kuwanoa madaktari wa hapa nchini.

No comments:

Post a Comment