MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesitisha huduma zote za mawasiliano zinazofanywa na Kampuni ya Six Telecoms Tanzania Limited kutokana na kuisababishia serikali hasara ya Dola za Marekani milioni 7.7 (Sh bilioni 15).
Pia, kampuni hiyo inadaiwa kufanya udanganyifu katika tozo za huduma za simu za kimataifa, kwa kutoa tozo ya chini zaidi ya bei elekezi ya mamlaka hiyo. Hatua ya TCRA imekuja baada ya kufanya ukaguzi wa kushtukiza kwa kampuni hiyo iliyopewa leseni ya mtandao na miundombinu.
Akizungumza wakati wa operesheni hiyo ya ukaguzi, Wakili Mwandamizi Mkuu wa TCRA, Johannes Kalungura alisema: “Mamlaka inasitisha huduma zote za Kampuni ya Six Telecoms Tanzania Limited, kwa sababu imekiuka sheria za nchi, kufanya udanganyifu wa tozo za huduma za simu za kimataifa na kushindwa kutekeleza maagizo wanayopewa na mamlaka hayo.” Alisema, kwa mujibu wa takwimu za TCRA, Six Telecoms Tanzania Limited imeisababishia hasara serikali Dola za Marekani milioni 7.7 kutokana na huduma za simu za kimataifa na huduma nyingine za mawasiliano zinazotolewa na kampuni hiyo.
Aliongeza, “Sasa tumezima mtambo na kuchukua baadhi ya vifaa kwa ajili ya uchunguzi kabla ya kulifikisha suala hilo katika vyombo vya sheria, hivyo wateja wa kampuni hii wajue hakutakuwa na huduma mpaka itakapoamuliwa vinginevyo.”
Hata hivyo, baada ya kufanya ukaguzi huo, Jeshi la Polisi lilimshikilia Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Rashid Shamte kwa ajili ya kuchukua maelezo yake kabla ya hatua nyingine.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, Shamte alionekana kuwa mkali kwa maofisa wa TCRA huku akikataa kusikiliza maelezo ya viongozi hao na kuona kuwa suala hilo angeweza kulimaliza kwa muda mfupi.
Akizungumza baada ya kuondoka katika ofisi zake, chini ya ulinzi wa Polisi, Shamte alisema tayari alishakutana na uongozi wa TCRA na kuzungumzia matatizo hayo na kuwa ameshalipa malimbikizo ya malipo kama walivyoagizwa na mamlaka hiyo, bila kutaja kiasi.
No comments:
Post a Comment