Thursday, 7 January 2016

Shehena Ya Petroli FEKI Yakamatwa.....Aserikali Yaamuru Irudishwe Ilikotoka!

 

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), limeamuru shehena ya mafuta ya petroli iliyoagizwa kutoka Falme za Kiarabu irejeshwe ilikotoka kutokana na kubaini hayana ubora unaotakiwa kwa matumizi ya magari na mitambo.

Akitoa taarifa hiyo Dar es Salam jana, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Joseph Masikitiko alisema, vipimo vya maabara vya sampuli ya mafuta hayo vimeonesha kuwa hayafai kwa matumizi.

Alisema hayo ni matokeo ya ukaguzi wa hivi karibuni wa shehena hiyo yenye ujazo wa tani za metriki 38,521.018 katika meli ya MT. Ridgebury John B, yaliyokuwa yasambazwe na kuuzwa nchini.

Alisema, "Vipimo vinaonesha kuwa baadhi ya matakwa ya viwango vya mafuta ya petroli hayajafikiwa, hivyo kuamuru yarejeshwe yalikotoka. Kiwango cha ubora cha mafuta ya petroli ni TZS 672:2012/ EAS 158:2012 ambacho hakikufikiwa".

Matakwa ya kiwango ambacho mafuta hayo hayakukidhi ni pamoja na kuwa na kemikali zilizo na oksijeni ndani yake ambazo husababisha madhara kwenye injini za magari na mitambo.

Alisema, "Kiwango cha petroli hakiruhusu uwepo wa kemikali hizo kwenye mafuta hayo kwa sababu zinaua injini, kuhatarisha afya za watu na kuharibu mazingira kutokana na kusababisha moshi mchafu mwingi".

Alifafanua kuwa mafuta hayo yameonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kuvuta maji au mvuke na kuwa sehemu ya petroli, kiasi cha kuifanya iwe na maji mengi ambayo ni hatari kwa injini za magari na mitambo.

Pia, alieleza uhafifu mwingine katika mafuta hayo kuwa ni kupungua kwa nguvu ya kuendesha injini au mitambo hivyo kusababisha uharibifu na hasara. 
Aliongeza kuwa, mvuke unapokuwa mwingi kwenye petroli husababisha mtiririko wa mafuta kwenda kwenye injini kutokuwa mzuri, huku kemikali aina ya benzene iliyoonekana kuzidi katika petroli hiyo ikiwa ni chanzo cha kansa kwa wanaotoa huduma ya uuzaji wa mafuta hayo.

Sambamba na hayo, Masikitiko aliongeza kuwa walibaini kuwa uhafifu katika mafuta hayo unaongeza wingi wa ujazo wa nishati hiyo pasipokuwa na uhalisia na kisha kutoa nguvu isiyolingana na wingi wake. Alisema, madhara yake ni mnunuzi kulipia wingi wa mafuta usio na thamani halisi.

Aliwahakikishia watumiaji wa mafuta kuwa, shirika hilo litahakikisha linafanya ukaguzi katika meli zote zenye mafuta yanayokusudiwa kusambazwa nchini ili kuzuia yasiyo na ubora yasiingizwe sokoni.

Katika hatua nyingine, Tbs ilisema kuwa iliagiza vilainishi vya mitambo na magari vya kampuni ya HASS Petroleum (T) Limited vyenye ujazo wa lita 16,080 kutoka Falme za Kiarabu virejeshwe vilikotoka pia kwa sababu ya kukosa ubora unaofaa kwa matumizi na kwamba mwagizaji alitekeleza agizo hilo tangu Desemba 31 mwaka jana.

Ewura yazungumza
 Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) imekiri kufahamu kuhusu suala hilo na kueleza wananchi kuwa licha ya mafuta hayo kutakiwa kurejeshwa yalipotoka, bado nchi ina akiba ya petroli inayoweza kutumika hadi shehena nyingine iletwe.

"Wananchi wasiwe na wasiwasi," alisema Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa Ewura, Titus Kaguo. Alisema kwa siku nchi inatumia lita za petroli 2,700,000, na kwamba kila metriki tani moja ya petroli huwa na lita 700,000.

"Kwa maana hiyo, lita 33,000,000 za petroli zilizokuja na kukataliwa endapo zingeshushwa na kutumika nchini zingeweza kutosheleza mahitaji kwa zaidi ya siku saba," alisema Kaguo .
 Hata hivyo, aliongeza kuwa si mafuta yote yanayoingia na meli bandarini hushushwa kwa ajili ya matumizi ya nchi, bali mengine huwa safarini kwenda nchi nyingine.

No comments:

Post a Comment