Monday, 18 January 2016

Mafuriko yawakosesha 700 mahali pa kuishi

Image result for mafuriko dodoma

MAFURIKO makubwa yamekumba kata kadhaa, zilizo jirani na barabara ya Dodoma- Iringa manispaa ya Dodoma na Bahi na kusababisha zaidi ya watu 778 kukosa mahali pa kuishi kutokana na nyumba kuanguka. Mvua hizo zilizonyesha usiku wa kuamkia jana, zimeelezwa kuwa kubwa na kuleta mafuriko katika kata za Mpunguzi, Matumbulu, Nzuguni na Dodoma Makulu, zote za Manispaa ya Dodoma na Kata ya Kigwe wilaya ya Bahi.
Katika kata ya Dodoma Makulu, Diwani wa kata hiyo, Paschal Matula alisema nyumba 18 zimeanguka wakati Kata ya Nzuguni, kulikuwa na mafuriko makubwa yaliyovunja daraja upande mmoja.
Wakazi wa Kata za Mpunguzi na Matumbulu, walifunga barabara ya Iringa- Dodoma kwa zaidi ya saa 3 hadi viongozi wa wilaya ya Dodoma wakiambatana na polisi walipofika eneo hilo na kufungua baada ya kutoa ahadi ya serikali kushughulikia tatizo la daraja.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mpunguzi na Matumbulu, Dionis Samo, alisema kuwa nyumba 70 zilianguka na kuacha watu 300 hawana makazi pamoja na uharibifu mkubwa wa mali, ikiwemo vyakula.
Samo alisema maji yaliyovunja ukuta wa barabara, yaliingia kwa wingi kwenye makazi ya watu wakati wakiwa wamelala na kwa sababu nyumba nyingi zilikuwa za udongo zilianza kuanguka.
“Tatizo letu sasa linakuwa ni sugu kwani Januari mosi pia kuna nyumba 48 zilianguka na kufanya watu wengi kukosa makazi, unajua tatizo la hapa ni mkandarasi wa ujenzi wa barabara ya lami Dodoma – Iringa ambaye alijenga daraja dogo wakati walipohamisha barabara,” alisema Samo.
Mtendaji huyo alisema kwamba tatizo hilo walishalifikisha serikalini.
Diwani wa Kata ya Mpunguzi, John Matonya alisema mafuriko hayo yaliwakumba saa 4 usiku.
Alisema si mara ya kwanza kukumbwa na maafa hayo, kwani usiku wa kuamkia Januari mosi, pia nyumba 50 zilianguka na wakazi 87 wakakosa makazi.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kigwe wilaya ya Bahi, Paschal Sijila alisema kuwa nyumba 270 zilianguka katika kata yake na watu 460 hawana mahali pa kuishi.
“Tunaiomba Serikali kufika hapa na kuwatafutia watu mahali pa kuishi, hawana nyumba, vyakula vimesombwa na maji, kuku karibu 16 wamekufa na viongozi nilishawaambia wakaniahidi kuwa watakuja sasa bado nawasuburi,” alisema Sijila.

No comments:

Post a Comment