JESHI la Polisi Mkoani Iringa limewatia
mbaroni wahamiaji haramu 83, raia wa Ethiopia, waliokuwa wakisafirishwa na roli
Scania T478 DFE mali ya Frola Mwambenja kutokea Kongowe Dar es Salaam wakielekea
Kyela mkoani Mbeya.
Pamoja na wahamiaji hao, Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Iringa Peter Kakamba aliwaambia wanahabari jana kwamba jeshi
hilo linamshikilia pia dereva wa roli hilo, Hans Mwakyoma (28) mkazi wa Tukuyu
Mbeya na msaidizi wake Alex Adam (32) mkazi wa Mbeya mjini, kwa tuhuma za
usafirishaji wa watu hao.
Kamanda Kakamba alisema gari hilo
lilikamatwa na askari wa doria wa jeshi hilo majira ya saa 3.30 usiku katika
kijiji cha Mahenge kitongoji cha Kibotora, barabara kuu ya Iringa Mbeya likiwasafirisha
watu hao kuelekea Kyela ambako ni mpakani mwa Tanzania na Malawi.
“Lilipokamatwa roli hilo, dereva alisema
halina mzigo, lakini askari wetu walipolifungua walikuta watu hao wakiwa
wamelaliana, baadhi yao wakiwa na hali mbaya na wengine wakiwa wagonjwa,”
alisema.
Alisema baada ya kuwakamata, wahamiaji
hao walipewa chakula na wale walioonekana wagonjwa wamepatiwa matibabu wakati
taratibu zingine za kuwafikisha katika vyombo vya sheria zikiendelea.
“Jambo la kushangaza ni kwamba watu hao
walipakiwa katika gari hilo Kongowe jijini Dar es Salaam. Kila mtu anajua
Kongowe sio Ethiopia kwahiyo kuna swali la kujiuliza ni namna walivyofika Kongowe
hadi wakapata huduma ya kusafirishwa kuelekea wanakoelekea,” alisema.
Alisema biashara haramu ya usafirishaji
watu ni jipu kubwa linalohitaji nguvu ya
pamoja katika kutumbuliwa kwani inahusisha mtandao wa watu wengi ndani na nje
ya nchi.
Alisema katika kupambana na biashara
hiyo, taarifa fiche za kiintelejensia za jeshi hilo zinaelekea kuunasa mtandao wa
biashara hiyo na lengo hilo litakapofanikiwa wahusika wake watatumbuliwa majipu
hadharani.
Alisema watu hao wamekuwa wakiitia
gharama kubwa serikali kwani bada ya kuwakamata imekuwa ikilazimika kuwahudumia
na kuwasafirisha hadi watokako.
Kamanda Kakamba amewaagiza askari wa
jeshi hilo mkoani hapa kuwa makini zaidi katika kulishughulikia suala hilo na
mengine ya kihalifu kwani hataki mkoa wake uwe mmoja katika mikoa inayopitisha
watu hao.
No comments:
Post a Comment