MABINGWA Watetezi wa Kombe la Italia maarufu huko kama Coppa Italia, Juventus, Jana walitinga Nusu Fainali baada ya kuifunga Lazio 1-0.
Kwenye Fainali ya Coppa Italia Msimu uliopita, Juve iliibwaga Lazio na kubeba Kombe.
Bao la ushindi la Juve hapo Jana lilifungwa Dakika ya 66 na Beki Stephan Lichtsteiner ambae alikuwa Mchezaji wa Lazio kwa Misimu Mitatu kabla kuhamia Juve.
Bao hilo la Juve lilitokana na Shuti la Simone Zaza kupiga Posti na Kipa Etrit Berisha kushindwa kuokoa Mpira uliorudi na Stephan Lichtsteiner kuuwahi na kuukwamisha wavuni.
Juve walianza Msimu huu wakiwa wanasuasua lakini sasa wameshinda Mechi zao 10 za Serie A, ambayo wao ndio Mabingwa Watetezi, na sasa wapo Nafasi ya Pili ikiwa ni nafasi murua kwao kwa kutwaa Taji lao la 5 mfululizo la Italy.
Kwenye Nusu Fainali ya Coppa Italia, Juve watawavaa Inter Milan, walio chini ya Kocha Roberto Mancini, ambao Juzi waliichapa Napoli 2-0 na kutinga Nusu Fainali.
No comments:
Post a Comment