Saturday, 19 December 2015

Waziri awahi ofisini kushika wachelewaji


KASI ya mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tano, imeendelea kutikisa sehemu mbalimbali, ambapo katika Wizara wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, baadhi ya watumishi wameanza kuonja joto la viongozi hao kwa kutakiwa kuwahi kazini.
Jana Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee Dk Hamisi Kigwangalla aliwahi ofisini kwake na kuanza kufuatilia suala la nidhamu ya kujali muda wa kuwahi kazini kwa watumishi wa wizara hiyo.
“Wafanyakazi wana wajibu wa kuwahi kazini muda wa kazi asubuhi kama ilivyopangwa kwa mujibu wa taratibu za utumishi wa umma na kutoka baada ya muda wa kazi, hatuwezi kuendelea kuvumilia tabia ya watu kuendelea kumwibia mwajiri muda wa kufanya kazi.
“Sisi tumewahi kazini, Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na vionozi wengine, halafu watumishi wanachelewa, tumeonesha mfano, tunawahi na tunachelewa kuondoka,” alisema Dk Kigwangalla.
Kufungiwa nje Dk Kigwangalla aliamuru utakapokwisha muda wa kuingia kazini, walinzi wafunge geti na kutoruhusu waliochelewa kuingia, hadi atakapomaliza kusaini madaftari ya mahudhurio, kulingana na idara na vitengo vilivyopo wizarani hapo.
Idara hizo ni Utawala, Kinga, Mafunzo, Tiba, Udhibiti na Uhakiki Ubora, Mganga Mkuu, Uhasibu, Sera na Mipango, Wauguzi na Famasia na vitengo vya Sheria, Mawasiliano Serikalini na Tehama. Dk Kigwangalla alisema kuwa wanachokifanya ni kukomesha tabia ya uchelewaji, iliyogeuka endelevu kwa sababu watumishi wameajiriwa ili kuhudumia wananchi.
Alisema ufuatiliaji huo utakomesha tabia ya watumishi kuchelewa kufika kazini na kuondoka mapema kabla ya muda wa kazi. Vilevile, Dk Kigwangalla aliwataka watumishi wafanye kazi kwa kujitolea, kwa kuwa Tanzania itajengwa na zama za kazi ambazo viongozi watatoa mfano wa kuwahi kazini kwa watumishi. Kuhusu watumishi waliochelewa, Dk Kigwangalla aliagiza waandike barua za kujieleza kwake na azipate jana hiyo hiyo.
Kazi hiyo alimkabidhi Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Michael John. Katika kudhibiti tabia hiyo ya uchelewaji, Dk Kigwangalla alimwagiza Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Michael John amueleze kwa maandishi ni kwa nini wizara hiyo haijachukua hatua ya kuingia katika mfumo wa kidijitali wa kudhibiti wachelewaji.
Mfumo huo huwalazimu watumishi kutoa taarifa ya kuwasili ofisini kwa kuweka vidole au kadi katika mashine za kielektroniki wakati wa kuingia kazini, ambapo taarifa zao hurekodiwa na kuiwezesha ofisi kujua mtumishi amefika kazini saa ngapi na kama atatoka, ajulikane yupo wapi na kwa nini.
Dk Kigwangalla alisema kuwa amefikia hatua hiyo ya kusimamia kukomesha tabia ya uchelewaji kutokana na Wizara hiyo kulaumiwa kwa na urasimu, kumbe watumishi hawawahi kazini. Katika hatua nyingine, Dk Kigwangalla ameagiza maelezo ya kina ya watumishi wa afya nchi nzima kuanzia madaktari, wauguzi na wafamasia, kuhusu mfumo unaotumika kuhakikisha wamefika ofisini na wanafanya kazi ipasavyo.
PSPF wapewa siku saba Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji, ametoa siku saba kwa Mfuko wa Pensheni wa PSPF kuwalipa wastaafu stahiki zao. Dk Kijaji alitoa agizo hilo jijini Dar es Salaam jana wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika ofisi hizo.
Alisema hapo awali Serikali ilikuwa ikidaiwa Sh bilioni 177 na mfuko huo, lakini kati ya hizo serikali imeshalipa Sh bilioni 154 na kiasi cha Sh bilioni 70 zimetolewa kati ya Novemba na Desemba mwaka huu. Aliongeza kuwa anashindwa kuelewa kwanini mpaka sasa wastaafu hao, wanaendelea kupata shida na kuumia wakati fedha zimetolewa.
“Wastaafu ni watu waliopewa kipaumbele, hakuna sababu ya kuwaacha wateseke nachokiomba kwenu, agizo hilo la siku saba litekelezwe kwa wakati ili wastaafu hao wapatiwe stahiki zao na kuondoa usumbufu wanaoupata,” alisema Kijaji. Aliwaomba wastaafu hao kuwa na subira kwani ndani ya siku hizo saba, watarajie kulipwa stahiki zao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Adam Mayingu alisema kuchelewa kwa malipo hayo, kumetokana na kucheleweshwa kwa michango ya wanachama kutoka serikalini, ambapo mpaka sasa Serikali inadaiwa michango ya miezi saba ambayo haijafika katika taasisi hiyo.
Alisema hadi sasa hundi 444 za kuanzia Aprili mpaka Oktoba kwa wastaafu 302 zimeshatayarishwa na kuahidi kuwa Serikali itakapowasilisha michango iliyobaki, wanachama wastaafu wote watalipwa. Imeandikwa na Eleuteri Mangi (MAELEZO) na Sophia Mwambe.

No comments:

Post a Comment