MBUNGE wa Simanjiro mkoani Manyara, James ole Millya (Chadema), amesema ipo haja ya kutunga sheria ndogo itakayowabana wachimbaji wakubwa na wadogo wa tanzanite katika machimbo ya Mererani wilayani humo, walipe kodi na tozo mbalimbali za halmashauri. Millya alisema ni vyema sasa kuangalia upya sheria zilizopo na kufanya marekebisho kwa kutunga sheria ndogo ili kuwabana wachimbaji na kampuni ya uwekezaji waweze kulipa tozo na kodi za halmashauri, vinginevyo mwisho wa siku wataachiwa mashimo matupu.
Alitoa kauli hiyo juzi wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa jimbo lake kwenye Ibada ya Misa ya shukrani, aliyoiandaa baada ya kushinda nafasi ya ubunge katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Katika uchaguzi huo, Millya alimwangusha aliyekuwa Mbunge maarufu wa jimbo hilo kwa miaka 10, Christopher ole Sendeka (CCM) ambaye aliongoza kati ya mwaka 2005/2015. Ibada hiyo ya misa ilifanyika katika uwanja wa wazi uliopo katika mji wa Orkesmet ambao ni Makao makuu ya jimbo hilo lenye utajiri mkubwa wa rasilimali.
Alisema umefika wakati sasa wa madini hayo kuwanufaisha wananchi wa Simanjiro badala ya mikoa mingine na hata nchi za mbali kama India na Afrika Kusini. Alisema halmashauri inapaswa iwe na wigo mpana wa kukusanya mapato ya ndani kutoka vyanzo kama migodi ya Tanzanite, Vitalu vya Uwindaji, Mashamba makubwa ya wawekezaji na vyanzo vingine .
Mbunge huyo alisema sheria hiyo ndogo itakayotungwa na Baraza la Madiwani itasaidia kuinua na kuongeza mapato. Pia fedha hizo zitaelekezwa moja kwa moja katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta zote nyeti kama vile elimu, maji, afya na miundombinu.
Alisisitiza kuwa kuanzia sasa atasimamia kwa nguvu zake zote kuzuia uuzaji wa ardhi katika wilaya ya Simanjiro, suala ambalo limewaathiri wakulima na wafugaji. “Sehemu kubwa ya ardhi ya jimbo letu imemegwa katika njia isiyo halali kwa watu waliobatizwa jina la wawekezaji, ambao hawatumii ardhi hiyo bali wameihodhi tu huku wananchi wetu wakiwa hawana ardhi ya kufanyia shughuli zao za kiuchumi kama kilimo na ufugaji kwa hiyo kuanzia sasa hatutaruhusu ardhi kuchukuliwa tu bila utaratibu unaoeleweka,”alisema.
Awali Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) kutoka Dayosisi ya Morogoro Paul ole Memeo aliwataka wananchi wa Simanjiro kushirikiana na mbunge kuijenga Simanjiro mpya. Aliwataka kuweka itikadi za kisiasa pembeni na kufanya kazi na Mbunge ambaye sasa ni kiongozi wa wananchi wote.
Ibada hiyo ya Misa ilihudhuriwa na wabunge wa Chadema, Onesmo Nangole (Longido), Dk Godwin Mollel (Siha) na madiwani wa kata zaidi ya 14 .
No comments:
Post a Comment