Monday, 21 December 2015

HIZI NI KAMPUNI 27 ZA tanzaniteAMBAZO ZIMEKWEPA KODI SOMA ZAIDI .......



 KAMPUNI 27 za kununua na kuuza madini ya tanzanite mkoani Arusha zilizosajiliwa, zinachunguzwa na serikali baada ya kubainika kukwepa kodi ya zaidi ya Sh bilioni 150 na ziko hatarini kufutiwa leseni.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mikoa mitatu ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara, Amos Makalla alisema uchunguzi wa awali umegundua wafanyabiashara hao sio waaminifu katika kufanya biashara zao za madini kwani wamekwepa kulipa mabilioni ya kodi serikalini.
Makalla ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro alisema katika uchunguzi wao na vikao vyao vya Desemba 10 na Desemba 17, mwaka huu, kamati hiyo maalumu ilibaini mambo mengi makubwa juu ya udanganyifu na wizi mkubwa unaofanywa na wafanyabiashara wa tanzanite katika kukwepa kodi.
Alisema katika kufanya upekuzi wa kina wenye kujiridhisha, walibaini kuwa tayari kampuni 27 zimekwepa kulipa kodi hiyo ya Serikali ya zaidi ya Sh bilioni 150 tangu mwaka 2013/14. Kutokana na hali hiyo, alisema wametoa muda kwa kampuni za kununua na kuuza madini, madalali na wachimbaji kujisalimisha kwa kulipa kodi hadi Januari 5, mwakani vinginevyo serikali itachukua hatua kali za kisheria.
Alisema baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wa tanzanite, madalali na wachimbaji wa madini hayo zaidi ya 5,000 wa Arusha, Manyara na Kilimanjaro sio waaminifu katika nyaraka zao za mapato na matumizi ya kila siku.
Kwa mujibu wa Makalla, katika nyaraka zao zinaonesha kutumia kiasi kikubwa cha fedha (returns) kila siku, lakini hawaoneshi kulipa kodi hata pale wanapopata madini na kutilia shaka nyaraka hizo.
Alisema kamati imejiridhisha na hali halisi ya ukwepaji kodi unaofanywa na wafanyabiashara wa tanzanite ambao wamekuwa wakifanya Mirerani (kunakochimbwa madini hayo pekee yanayopatikana Tanzania) kama shamba la bibi la kuvuna bila ya kulipa kodi sasa mwisho wa wafanyabiashara hao umefika.
“Nataka kukuambia kuwa kutatokeo mtikisiko mkubwa sana ambao haujawahi kutokea katika miaka mingi hapa nchini hususan hawa wafanyabiashara wa tanzanite kwani wamefanya Mirerani ni shamba la bibi la kuvuna mabilioni ya fedha bila ya kulipa kodi,” alisema Makalla na kuongeza:
“Wakati wa wafanyabiashara wa tanzanite kukwepa kulipa kodi umekwisha, wanapaswa kujisalimisha wenyewe kwa kulipa kodi vinginevyo rungu la dola litawasaka walipo.”
Akizungumzia wageni kufanya kazi na kujaa migodini, alizitaka kampuni zote ziwe kubwa ama ndogo kuwaondoa wafanyakazi wote wasio na kibali kabla ya operesheni haijaanza baada ya Januari 5, mwakani.
Alisikitishwa kuona kazi zinazopaswa kufanywa na Watanzania zinafanywa na raia wa nje wakiwamo kutoka Kenya na bara Asia, zikiwamo za ulinzi migodini.

No comments:

Post a Comment