Saturday, 26 December 2015

Dar ina maeneo ya wazi 180 yaliyovamiwa’



JIJI la Dar es Salaam lina maeneo ya wazi 180 ambayo yamevamiwa, ambapo 111 yapo Halmashauri ya Kinondoni, 50 yapo Ilala na Temeke yapo 19. Hayo yamebainishwa wakati Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba, walipozungumza na waandishi wa habari.
Makamba alifafanua kuwa Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 imeweka makatazo mahsusi kwa nia ya kuepusha uharibifu wa mazingira, ambapo Kifungu cha 57 cha sheria hiyo, kinazuia shughuli zozote zinazoweza kuhatarisha au kuathiri mazingira kutofanyika ndani ya mita 60 katika kingo za mito, maziwa na bahari ili kulinda maeneo hayo.
“Tunawaomba wale wote waliokiuka sheria hii, wabomoe wenyewe, vinginevyo tutaanza kubomoa wenyewe na hatutamuonea huruma mtu,kwa sababu mazingira yameharibiwa sana”, alisema Makamba.
Alisisitiza kwamba wale wote waliojenga kwenye fukwe, na kingo za maziwa na bahari, waanze kuondoka wenyewe, kwa sababu wizara inaanza kutekeleza sheria ya mazingira kikamilifu.
“Tukimaliza kubomoa maeneo ya ufukweni na kwenye kingo za mito na maziwa nchi mzima , tutahamia kwenye maeneo ya wazi, watu waondoke wenyewe wasingoje kubomolewa,” alisisitiza Makamba.
Kwa upande wake, Lukuvi alisema kuanzia Januari mwakani ataongoza kazi ya kugawa vipisi vya ramani za maeneo kwa wenyeviti wa serikali za mitaa nchini, zinazoonesha matumizi ya ardhi kwa eneo husika.
Alisema eneo la bonde la mto Msimbazi, linalokadiriwa kuwa na ukubwa wa ekari 1,927 mara baada ya bomoabomoa kumalizika, eneo hilo linaandaliwa kwa ajili ya kutengenezwa maeneo ya burudani kwa umma.
Alisema eneo hilo ni kuanzia daraja la Selander hadi Vingunguti pamoja na maeneo mengine ya bonde hilo. Lukuvi alisema serikali imesimamisha kazi ya bomoabomoa kwa siku 15, kwa wavamizi waliojenga katika Bonde la Mto Msimbazi na kuwataka wavamizi hao kubomoa wenyewe na kuondoka maeneo hayo kabla ya kazi hiyo kuanza tena Januari 5 mwakani.

No comments:

Post a Comment