+
WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imesimamisha kazi ya
bomoabomoa kwa siku 15 kwa wavamizi waliojenga katika Bonde la Mto
Msimbazi, Dar es Salaam na kuwataka wavamizi hao kubomoa wenyewe na
kuondoka maeneo hayo, kabla ya kazi hiyo kuanza tena Januari 5, mwakani.
Aidha, wale wote waliojenga kwenye maeneo ya wazi, wavamizi wa maeneo
ya watu, maeneo ya shughuli za kijamii kwenye fukwe, kingo za mito na
vyanzo vya maji nchi nzima, kazi ya ubomoaji itaanza mapema Januari
mwakani na kwamba hakuna atakayefidiwa.
Hayo yalibainishwa jana Dar es Salaam na Waziri wa Wizara hiyo,
William Lukuvi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na
Mazingira, January Makamba, wakati wakizungumza na waandishi wa habari.
Lukuvi alisema wameamua kusimamisha kwa muda kazi hiyo ili kutoa
nafasi kwa wavamizi hao kubomoa wenyewe nyumba walizojenga kinyume cha
sheria ili waambulie vitu vyao na baada ya muda uliotolewa kumalizika,
kazi ya ubomoaji itaendelea na hakuna atakayelipwa fidia.
Alisema katika eneo hilo la Bonde la Mto Msimbazi, nyumba 8,000
zimejengwa isivyo halali na hadi sasa nyumba 395, zimebomolewa kwa siku
tatu kuanzia Desemba 17 na kwamba wavamizi hao wasitegemee kulipwa
fidia.
“Hakuna fidia kwa wavamizi hao, kama huku nyuma kuna watu walionewa
huruma kwa sababu ya maafa na kupewa viwanja, ilikuwa ni huruma tu,
hakuna sheria inayomruhusu mtu kujenga kwenye eneo hatarishi, hivyo
tutakuondoa tu na hakuna fidia,” alifafanua Lukuvi.
Alisema hakuna nyaraka zilizotolewa kwa wavamizi hao kujenga maeneo
hayo, na kama kuna mtu ana kibali cha ujenzi kwenye eneo hilo hatarishi
au kingo za mto, sheria ya mazingira itamuondoa na hakuna watakaoachwa.
Kwa upande wake, January alisema Sheria ya Mazingira iko wazi na
inakataza watu kufanya shughuli kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kwa sababu
za kulinda mazingira na vyanzo vya maji.
Alisema kuanzia mwakani, wizara hiyo itaendesha operesheni ya
kuwaondoa watu wanaoishi na kufanya shughuli kwenye maeneo ya kingo za
mito na maziwa, fukwe za bahari, maeneo oevu na maeneo ya wazi. Kwa Dar
es Salaam, maeneo ya wazi 180 yamevamiwa, kati ya hayo 111 yapo
Halmashauri ya Kinondoni, 50 yapo Ilala na Temeke yapo 19.
No comments:
Post a Comment