PAZIA la kuwania nafasi ya Spika na Naibu Spika kupitia Chama Cha
Mapinduzi, limefungwa jana saa kumi jioni katika Ofisi Ndogo ya chama
hicho Lumumba jijini Dar es Salaam, huku wanachama waliojitokeza kuwania
nafasi hizo wakibakia wale wale 22 wa juzi.
waandishi wa habari walipiga kambi katika ofisi hizo tangu asubuhi mpaka
kipenga cha mwisho kwa siku nzima jana, lakini hakukuwa na mgombea hata
mmoja aliyeongezeka kuchukua fomu ya kuwania nafasi hizo. Katibu wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Oganaizesheni, Mohamed Seif
Khatib, alikuwepo tangu asubuhi katika ofisi hizo kusubiri kama
kungekuwa na nyongeza ya wagombea wa nafasi hiyo na ilipofika saa kumi
kamili, alifunga ofisi na kuondoka.
Juzi akizungumza katika ofisi hizo, Khatib alisema utaratibu wa
uchukuaji fomu ulitoa nafasi kwa aina mbili ya wanachama wanaowania
nafasi hizo; wale ambao ni wabunge na ambao si wabunge. Kwa wanachama
ambao si wabunge, walipewa nafasi ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi
hizo kwa siku mbili za Jumatano na Alhamisi, ili kutoa nafasi ya fomu
zao kwenda Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwa ajili ya uhakiki wa sifa
zao.
Kwa utaratibu huo, pazia la uchukuaji fomu kwa wanachama wasio
wabunge, lilifungwa Alhamisi iliyopita na wanachama ambao ni wabunge
walipewa nafasi mpaka jana saa kumi, ili kutoa nafasi ya uamuzi wa vikao
vya juu vya CCM. Waliochukua fomu Waliochukua fomu kuwania nafasi ya
Spika ni pamoja na aliyekuwa Naibu Spika katika Bunge la 10 na Mbunge wa
Kongwa, Job Ndugai, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Tulia Arkson
na aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi.
Wengine ni Spika mstaafu, Samuel Sitta, Mbunge mteule wa Chato, Dk
Medard Kalemani, Diwani wa Goba, Dar es Salaam, Mwakalika Watson, Julius
Pawatila, Agnes Makune, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Abdullah
Ali Mwinyi, Mbunge wa zamani wa Afrika Mashariki, George Nangale, Simon
Rubugu, Banda Sonoko na Leonce Mulenda. Pia yumo aliyewahi kuwa Naibu
Waziri, Ritha Mlaki na mhitimu wa chuo kikuu mwenye umri wa miaka 28,
Veraikunda Urio.
Kadhalika yupo aliyekuwa mbunge wa Karagwe, Gosbert Blandes na
aliyekuwa mmoja wa wagombea 42, waliojitokeza kuwania nafasi ya urais
ndani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Dk Kalokola Muzzamil.
Wengine ni aliyekuwa Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi,
aliyewahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na
Bunge, Philip Marmo, Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Italia, Profesa
Costa Mahalu na Mbunge mteule wa Kasulu Mjini, Daniel Nsanzugwanko.
Naibu Spika mmoja Kati ya wanachama wote waliojitokeza wakiwemo
vigogo wenye uzoefu mkubwa na wasio vigogo, ni mmoja tu Mbunge wa Ilala,
Mussa Azzan Zungu, aliyechukua fomu ya kuwania nafasi ya Naibu Spika.
Kwa uzoefu wake, Zungu angeweza kuongeza joto katika nafasi ya Spika,
ambako baadhi ya wagombea waliojitokeza hawana sifa na uzoefu wake,
lakini badala yake amekuwa mgombea pekee aliyejitokeza kuwania nafasi ya
Naibu Spika.
Zungu mbali na kuwa mbunge kwa kipindi cha pili sasa, pia ana uzoefu
katika uongozi wa kamati za kudumu za Bunge na wa kuongoza vikao vya
Bunge katika nafasi ya Mwenyekiti wa Bunge la 10. Akizungumza na gazeti
hili kuhusu hatua hiyo ya Zungu, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam, Profesa Benson Bana, alisema mgombea huyo amewania nafasi
ambayo inamfaa, kwa sababu ana uzoefu.
“Huyu amegombea nafasi anayoiweza, na amefanya vizuri kuomba,
anastahili iwapo ataipata,” alisema Profesa Bana. Gazeti hili liliripoti
kuwa juzi liliripoti kuwa Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM),
alionekana kufanya kampeni kwa wabunge wenzake na alipoulizwa na gazeti
hili, alisema moja kwa moja kuwa Naibu Spika anayefaa ni Zungu.
Washindani Akizungumzia mchuano kati ya wagombea wa nafasi ya Spika,
Profesa Bana alisema wapo wagombea wenye uzoefu na wengine wamewania
nafasi hiyo kwa kutaka majina yao yasikike, ili wajiandalie njia kwa
miaka ijayo. Akifafanua zaidi, Profesa Bana alisema nafasi ya Spika
ambayo imeombwa na wanachama 21, baadhi yao wameiomba tu kwa lengo la
majina yao kusikika ila wapo wenye nia ya kweli ya kuitaka.
Akichambua aina ya wagombea hao, alisema yupo mmoja ambaye ameomba
nafasi hiyo kwa kuwa alikuwa katika nafasi za juu katika mabunge
yaliyopita na huyo akasema amefanya jambo jema. Mbali na huyo aliyeshika
nafasi za juu katika mabunge yaliyopita, pia Profesa Bana alisema yupo
mwingine ambaye ana uzoefu usiotia shaka na analielewa Bunge hivyo
akiipata nafasi hiyo, ni sahihi pia.
Anayejisafisha Profesa Bana pia alisema kati ya wagombea hao wa
nafasi ya Spika, yupo mmoja ambaye anaonekana lengo lake ni jina lake
lisife, kwa kuwa hapo awali aliwahi kuhitilafiana na uamuzi muhimu wa
vikao chama. Wasafisha nyota Kwa mujibu wa Profesa Bana, wagombea
wengine waliowania nafasi hiyo wanajitengenezea njia mwenye miaka ijayo
kwani kwenye siasa wenye nia za kuwania nafasi mbalimbali huanza
maandalizi mapema.
“Mfano utaona hata Rais mstaafu Jakaya Kikwete, alianza kuonesha nia
ya kuwania urais mwaka 1995, mwaka huu pia wapo walioonesha nia ila si
kama waliutaka kwa sasa, ni kutengeneza njia ya miaka ijayo,” alisema
Profesa Bana. Sitta bungeni Katika hatua nyingine, Sitta jana alitinga
viwanja vya Bunge mjini Dodoma na kusalimiana na wabunge mbalimbali.
Sitta alifika katika viwanja hivyo majira ya saa tano asubuhi, ambapo
shughuli ya wabunge kujisajili kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano wa Bunge
la 11 litakaloanza Jumanne ijayo ilikuwa ikiendelea kwa siku ya pili
mfululizo. Alipoonekana eneo hilo kundi la waandishi wa habari
wanaoripoti habari za Bunge walimfuata kutaka kuzungumza naye na
kumuuliza maswali mbalimbali.
Lakini Sitta, ambaye mara kwa mara anapofuatwa na waandishi wa habari
katika mazingira kama hayo huwa mwepesi kuzungumza, aliwajibu
wanahabari kwamba wampe kwanza nafasi. “Niacheni kwanza ndugu zangu
nifanye kazi iliyonileta hapa,” alisema na kuelekea katika meza
mbalimbali ambako kulikuwa na makundi ya wabunge wamekaa. “Naitwa Samuel
Sitta, nawania uspika,” alisikika akijitambulisha katika baadhi ya meza
huku akitaniana na wabunge wa siku nyingi, lakini pia akipata fursa ya
kufahamiana na wabunge wapya.
Baada ya kusalimiana na baadhi ya wabunge wapya waliofika jana
kujiandikisha, lakini pia kubadilishana mawazo na wabunge mbalimbali
wakiwemo wale waliokuwa Bunge la 11 lililomalizika Agosti 21 mwaka huu,
waandishi walimfuata tena kutaka kuzungumza naye, lakini safari hii
mmoja kati ya wasaidizi wake alisema unaandaliwa utaratibu wasiwe na
haraka.
Tukio hilo lilifanya baadhi ya wanahabari kuanza kuona pengine
kungekuwa na ugumu jana kwa Sitta aliyekuwa pia Mwenyekiti wa Bunge
Maalumu la Katiba, kwamba hakuwa na mpango wa kuzungumza na wanahabari.
Baadaye majira ya saa saba mchana, msaidizi huyo aliwaambia waandishi wa
habari: “Naomba mumsubiri mzee, anaingia ofisini kidogo kisha atarudi.”
Lakini baada ya tangazo hilo, Sitta alitoka eneo la viwanja hivyo na
kuondoka akiwaacha wanahabari wamepigwa na butwaa bila kuzungumza naye
kwa kina. Sitta aliyehudumu pia nafasi ya Spika wa Bunge la Tisa
lililokuwa likijulikana kama la kasi na viwango, ni miongoni mwa makada
zaidi ya 20 wa CCM walioomba kuteuliwa na chama hicho kuwania nafasi
hiyo.
Muombaji huyo wa nafasi hiyo hakuwania ubunge wa jimbo la Urambo
Mashariki alilolitumikia hadi Bunge lilipovunjwa mwaka huu, ambapo
ameshika nyadhifa mbalimbali za Uwaziri katika Awamu ya Pili ya Serikali
na ya Awamu ya Nne, akimalizia na Wizara ya Uchukuzi. Kwa mujibu wa
ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Bunge, kuanzia juzi hadi leo ni usajili
wa wabunge kwa ajili ya kushiriki mkutano huo, wakati kesho saa nne
asubuhi hadi saa sita mchana itakuwa kikao kwa wabunge na pia kutembelea
ukumbi wa bunge, ambapo alasiri itakuwa mikutano ya kamati za vyama.
Jumanne itakuwa ni kuanza kikao cha kwanza cha Bunge na kusomwa
tangazo la Rais la kuitisha Bunge, Uchaguzi wa Spika, kiapo cha Spika,
wimbo wa Taifa kupigwa na baadaye wabunge wataanza kuapishwa hadi
Alhamisi asubuhi. Alhamisi jioni itakuwa kuthibitisha jina la Waziri
Mkuu na pia baadaye Uchaguzi wa Naibu Spika, wakati Ijumaa alasiri Rais
Dk John Magufuli atahutubia bunge na baadaye itatolewa hoja ya
kuahirisha Bunge.
Massaburi ajitoa Katika hatua nyingine, habari kutoka mjini Dodoma
zinasema kuwa aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Massaburi
amejiondoa katika kinyang’anyiro hicho cha kuwania Uspika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ili kujenga umoja na mshikamano ndani
ya chama. Habari za kuaminika zilieleza jana kwamba Dk Massaburi alikuwa
katika mpango wa kuandika barua kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman
Kinana ili kumweleza azma yake ya kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho
kama kielelezo cha kuonyesha umoja na mshikamano ndani ya chama hicho
tawala.
“Ni kweli zipo taarifa kwamba wakati Kamati Kuu inakutana leo, Dk
Massaburi amefikia uamuzi wa busara wa kuondoa jina lake. Na ikumbukwe
kwamba yeye si wa kwanza kwani hatua kama zake za kujiondoa zimewahi
kuchukuliwa na wagombea wengine miaka ya nyuma hatua ambayo ilikisaidia
sana chama kujenga mshikamano na hatimaye kushinda kwa kishindo.
“Bado hatujapokea rasmi barua yake lakini mara baada ya kuipokea
tutatoa taarifa rasmi juu ya uamuzi wake huo, lakini taarifa zake
tumeshazipokea ndani ya Sekretarieti ya chama hapa Dodoma,” alisema
mmoja wa maofisa wa Ofisi ya CCM Makao Makuu Dodoma, ambaye hakutaka
jina lake kutajwa gazetini hadi taarifa rasmi ya chama itakapotolewa.
Hadi jana wakati wabunge wakiendelea kujiorodhesha kwenye ofisi za
Bunge tofauti na wagombea wengine ambao walionekana mjini humo wakiomba
kura, Dk Massaburi hakuonekana. Alipopigiwa simu kuhusu kuwepo kwa
taarifa za kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho, ingawa hakutaka
kueleza kwa kina suala hilo alisema alikuwa akiendelea kufanyia kazi
lakini yupo tayari kuchukua uamuzi wowote ambao utaonekana kuijenga CCM
na kuleta umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama wake.
“Nitatoa taarifa zaidi kesho (leo) inawezekana ikawa hivyo au isiwe
hivyo lakini kama mnavyojua ni kwamba kinachotakiwa ni kupatikana kwa
mwanaCCM mwenye uwezo na uzoefu katika kuiendesha taasisi ya Bunge.
“Naamini mimi pia uwezo wangu ni mkubwa lakini katika kuheshimu dhana ya
kuzidiana na hata kuheshimu uwezo wa wengine, nipo tayari kwa lolote.
“Kwa mfano mtu kama (anamtaja mmoja wa wagombea) ameomba kugombea
nafasi ya uspika kwa hiyo katika muktadha huo huo wa kuhakikisha Bunge
linakuwa na kiongozi mahiri na mzoefu, nitakuwa tayari kumuunga mkono
ili aweze kushinda nafasi hiyo na kuliongoza Bunge chini ya Rais
Magufuli.
“Watanzania wote wana hamu ya kuona kuwa anapatikana Spika anayeweza
kwenda na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano,” alisema Dk Massaburi.
Imeandikwa na Amir Mhando, Dodoma na Regina Kumba na Ikunda Erick, Dar.
No comments:
Post a Comment