Mh spika wa bunge la 11 Job Ndugai |
MBUNGE wa Kongwa mkoani Dodoma, Job Yustino Ndugai (55) ndiye Spika
mpya wa Bunge atakayeongoza Bunge la 11 lililoanza mkutano wake wa
kwanza jana. Ndugai, ambaye ni Mbunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
alichaguliwa kwa kishindo, akitwaa nafasi hiyo baada ya kuwashinda
wagombea wengine saba kutoka vyama vya siasa kwa kupata asilimia 70 ya
kura zote zilizopigwa.
Akitangaza matokeo hayo, Katibu wa Bunge ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi huo, Dk Thomas Kashilillah, alisema Ndugai aliyekuwa Naibu Spika katika Bunge la 10, alipata kura 254 akifuatiwa na mgombea wa Chadema, Goodluck Ole Medeye aliyepata kura 109, huku kura zilizopigwa zilikuwa 365 na kura mbili ziliharibika. Wagombea wengine sita na vyama vyao katika mabano ambao hawakupata kura ni Peter Sarungi (AFP), Hassan Almas (NRA), Dk Godfrey Malisa (CCK), Richard Lyimo (TLP), Hashim Rungwe (Chaumma) na Robert Kasinini (DP).
Kati ya wagombea hao wanane ni Ndugai peke yake ambaye ni Mbunge katika Bunge la 11, ambapo awali kabla ya upigaji kura kuanza, Mwenyekiti wa Kikao cha Uchaguzi ambaye ni Mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge (CCM) alilazimika kutoa hoja ya kutengua Kanuni ili wagombea ambao si wabunge waruhusiwe kuingia ukumbini.
Chenge aliteuliwa kuongoza kikao hicho kutokana na kuwa mbunge aliyekaa muda mrefu zaidi ambapo amekuwa bungeni tangu mwaka 1993 alipoteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati huo Rais akiwa Ali Hassan Mwinyi, kisha aliteuliwa tena mwaka 1995 katika nafasi hiyo hiyo wakati Rais akiwa Benjamin Mkapa, kabla ya mwaka 2005 kugombea ubunge Bariadi Magharibi nafasi anayoishikilia hadi sasa.
Kutokana na ushindi huo, Ndugai anakuwa Spika wa sita wa Bunge hilo akitanguliwa na Adam Sapi Mkwawa kuanzia 1964 hadi Novemba 19, 1973, kisha aliingia Erasto Mang’enya Novemba 20, 1973 hadi Novemba 5, 1975, kisha alirudi tena Mkwawa kuanzia Novemba 6, 1975 hadi Aprili 25, 1994. Wengine ni Pius Msekwa Aprili 28, 1994 hadi Novemba 20, 2005, Samuel Sitta Desemba 26, 2005 hadi Novemba 2010, kisha Makinda Novemba 12 hadi jana.
Baada ya kutangazwa mshindi, Mwenyekiti Chenge alimtaka atoke nje ya ukumbi kwenda kuvaa joho rasmi na kuingia tena ukumbini akiongozwa na maaskari wa Bunge na kisha kuapishwa na Katibu wa Bunge. Aahidi kutenda haki Akizungumza baada ya kukalia kiti hicho, Ndugai ambaye amekuwa Mbunge tangu mwaka 2000, aliwashukuru wabunge kwa heshima waliyompa na kuahidi kutenda haki kwa wabunge wote.
Aliwaeleza wabunge kwamba alipokuwa mdogo alizaliwa peke yake kwa mama yake, hivyo alikuwa kila wakati akimwambia mama yake aende zahanati akatafute mtoto mwingine ili awe na wenzake.
Baada ya hotuba yake, alianza kazi mara moja kwa kumwapisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, aliyefuatiwa na Mwenyekiti wa Kikao cha jana, Chenge na baadaye Mbunge wa Kuteuliwa, Dk Tulia Ackson (CCM). Aliwaapisha wabunge wengine wanne ambao ni Kabwe Zitto (Kigoma Mjini – ACT-Wazalendo), Dk Mary Nagu (Hanang – CCM), Richard Ndassa (Sumve – CCM) na Upendo Pendeza (Viti Maalumu – Chadema), kabla ya kuahirisha kikao hadi jana jioni alipoendelea na kazi ya kuapisha wabunge wengine.
. Katika hatua nyingine, wabunge watano wa CCM wamejitokeza kuwania nafasi ya Naibu Spika na walitarajiwa kupigiwa kura na wenzao jana jioni.
Hao ni Bahati Abeid, Mariam Kisangi, Sadifa Juma Khamis, Dk Tulia na Mussa Azzan Zungu. Uzoefu Ndugai bungeni Naibu Spika 2010-2015 Aliongoza vikao vya Kamati za Bunge kwa zaidi ya miaka 10 Mwenyekiti wa Kamati ya iliyotunga Kanuni za sasa za Bunge Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Bunge 2010-2015 Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi 2010-2015 Mwenyekiti Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii 2005-2010 Elimu Shahada ya Kwanza ya Sayansi katika Zoology (Chuo Kikuu cha Dares Salaam). Shahada ya Uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Norway katika uongozi wa Maliasili. Shahada ya Uzamili kutoka Chuo Kikuu cha ESAMI katika uongozi (MBA).
No comments:
Post a Comment