Andre Ayew |
Wengi wamekuwa
wakizungumzia ugumu wa kuzoea ligi kuu ya England, lakini Mghana André
Ayew alifanya hilo likose maana baada ya kutua kwa kishindo Swansea.
Bao la pili lilifuata akicheza mechi yake ya kwanza uwanja wa nyumbani, lakini ni ushindi wa 2-1 dhidi ya timu ya Manchester United mwishoni mwa mwezi Agosti uliotangaza kufika kwa Ayew.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 alisawazishia timu yake iliyokuwa imelezwa, kabla ya kusaidia kuunda bao la ushindi la Bafetimbi Gomis, kwa pasi safi kwa kutumia kisigino.
Muda si muda, mchezaji huyo ambaye alizaliwa na sifa za kiongozi alitawazwa mchezaji bora Ligi ya Premia wa mwezi Agosti na kusifiwa kama mojawapo ya nyota wazuri walionunuliwa msimu huu.
Ni jambo la kushangaza ikizingatiwa kwamba Swansea walikuwa wamesajili akiwa hana klabu yoyote.
Ayew, ambaye ni mtoto wa nguli wa mpira ulimwenguni Abedi 'Pele', Ayew, ana ustadi, uthabiti na ujanja mchezoni. Ni kana kwamba amefika nyumbani katika ligi aliyoitamani sana.
“Huu ulikuwa ndio wakati mwafaka kwangu kucheza katika Ligi ya Premia na kutimiza ndoto yangu,” aliambia BBC Sport.
“Nilizoea uchezaji wa hapa vyema kwa sababu niliingia mapema. Nilikuwa na mufa wa kujiandaa kipindi chote cha kabla ya msimu, nilifahamiana na wachezaji wenzangu, na wakanipa ujasiri na uwajibikaji.”
Na amejibu kwa kufunga mabao MATANO na kusaidia ufungaji wa bao MOJA katika mechi KUMI NA MOJA za kwanza alizocheza Ligi ya Premia.
Kuwasili kwake UIngereza kulitokea baada yake kuwa na msimu mbaya na Marseille, waliomaliza nafasi ya nne katika ligi kuu ya Ufaransa na kuondolewa kutoka mashindano mawili ya vikombe mapema.
Lakini Ayew, alifana bado, ustadi wake ukifanya asifiwe sana alipokuwa akiondoka katika klabu hiyo aliyojiunga nayo kama kijana baada ya kukaa miaka 11 na kushinda vikombe viwili vya ligi (na kufunga mabao 61).
Wakati alipokuwa akiwapa mkono wa kwaheri mashabiki wa Velodrome mnamo mwezi Mai, Ayew, aliyekata kipande cha zulia akahifadhi kama kumbukumbu, alishindwa kuzuia machozi pale mashabiki walipokuwa wakiliimba jina lake.
Na hiyo haikuwa mara yake ya kwanza kutokwa na machozi mwaka huu.
Mwezi Februari, alilia baada ya Ghana kukosa fursa ya kushinda Kombe la Taifa Bingwa Afrika mara ya kwanza katika miaka 33 waliposhindwa na Ivory Coast kupitia mikwaju ya penalti.
Ayew alifunga mkwaju wake na naibu nahodha huyu wa timu ya Ghana pia alimaliza kama mfungaji mabao bora, akishikilia nafasi hiyo pamoja na wachezaji wengine watano waliofunga mabao matatu.
Muhimu zaidi lilikuwa bao lake la ushindi la dakika ya 83 dhidi ya Afrika Kusini, mechi iliyokuwa ya mwisho kwa Black Stars kundini, iliyohakikisha wanamaliza kileleni katika kundi lao.
Alishinda tuzo ya BBC ya mwanakandanda bora wa Afrika wa mwaka 2011 lakini je, Ayew anaweza kuwa Mghana wa kwanza kushinda tuzo hii mara mbili?
No comments:
Post a Comment