WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema atahamia Dodoma ifikapo Septemba, mwaka
huu kuonyesha kuwa Serikali imedhamiria kutekeleza ahadi ilizotoa kwa
wananchi.
Ametoa
kauli hiyo leo asubuhi (Jumatatu, Julai 25, 2016) wakati akizungumza na
mamia ya wakazi wa mkoa wa Dodoma na kuwashukuru kwa ushiriki wao
kwenye maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa zilizofanyika
kwenye uwanja wa Mashujaa, mjini Dodoma.
“Jana
nilimwita Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na kumwambia akamilishe
matengenezo kwenye nyumba yangu kwa sababu ninataka kuhamia Dodoma
ifikapo Septemba,” amesema na kushangiliwa na mamia ya wakazi wa mji wa
Dodoma waliohudhuria maadhimisho hayo.
Amesema
tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, kazi nyingi
zimefanyika na wananchi wameziona na kwamba sasa hivi kazi iliyobakia ni
utekelezaji wa ahadi alizotoa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dk. John Magufuli.
“Wananchi
kazi mmeziona na sasa tunaenda kwenye utekelezaji. Ninatoa agizo kuwa
mawaziri na manaibu wote wahame mara moja kutoka Dar es Salaam na kuja
Dodoma. Wana ofisi ndogo Dodoma na kwa kuwa wamekuwa wakiishi wakati
wote wa Bunge, wahamie mara moja. Mimi nahamia Septemba, na utekelezaji
wake nitausimamia kwa juhudi zote,” alisisitiza.
Amewataka
wakazi wa Dodoma watumie fursa hiyo kutunza amani ya nchi na kudumisha
umoja uliopo na pia akataka watumie fursa hiyo kujenga nyumba za kuishi
za kutosha, nyumba za kulala wageni na hoteli za kitalii ili watu
watumishi na wageni wanapokuja wasipate taabu mahali pa kuishi.
Wakati
huo huo, mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli katika muda wa siku tatu
amerudia kusisitiza nia ya Serikali kuhamia Dodoma katika kipindi chake
cha uongozi ili kutekeleza ndoto ya hayati Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere ya kutaka makao makuu ya nchi yawe Dodoma.
Akizungumza
na mamia ya wakazi wa mji wa Dodoma kwenye uwanja wa mashujaa huku
akishangiliwa, Rais Magufuli amesema atahakikisha Dodoma inakuwa makao
makuu ndani ya miaka minne na miezi minne iliyobakia kwenye awamu ya
kwnza ya uongozi wake.
“Kama
wabunge karibu 300 na mawaziri na manaibu wao ambao hawafiki 30 wanakaa
hapa kwa miezi mitatu na maisha yanakwenda, kama makao makuu ya chama
kinachotawala nchi yako hapa sioni sababu ni kwa nini Serikali
ninayoiongoza iendelee kubakia Dar es Salaam,” amesema.
Mara
kwanza kutoa kauli hiyo, ilikuwa ni Jumamosi iliyopita, Julai 23, 2016
wakati akitoa hotuba yake ya kwanza mara baada ya kuchaguliwa kuwa
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Mkutano Mkuu maalum wa chama
hicho.
Rais
Magufuli amesisitiza wananchi na wanasiasa kutunza amani na kudumisha
amani iliyokuwepo nchini. Pia amewataka Watanzania wote kuendelea
kuwaenzi mashujaa walioipigania nchi hii.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMATATU, JULAI 25, 2016.
No comments:
Post a Comment