Thursday, 28 July 2016

Papa Francis aanguka akiongoza ibada Poland

Papa
Papa Francis aliendelea na misa bila kuonekana kuumia
Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis ameteleza na kuanguka alipokuwa akielekea kwenye altare kuongoza ibada ya misa nchini Poland.

Papa Francis alikosa kukanyaga vyema kidato kimoja na akaanguka katika madhabahu matakatifu zaidi nchini humo, madhabahu ya Jasna Gora.
Papa, mwenye umri wa miaka 79, mzaliwa wa Argentina, alionekana akitembea akiwa anatafakari sana, na hakugundua kulikuwa na kidato kimoja kabla ya kufikia altare, shirika la habari la AP limeripoti.
Mapadre waliokuwa karibu naye walikimbia na kumsaidia kuinuka.
Misa iliendelea kama ilivyopangwa na papa alihubiri kwa muda mrefu mbele ya maelfu ya waumini waliokusanyika Jasna Gora katika jiji la Czestochowa, kusini mwa nchi hiyo.
Shirika la habari la AFP linasema aliinuka upesi, na hakuonekana kuumia hata kidogo.
Alipoulizwa iwapo Francis aliumia baada ya kuanguka, msemaji wa Vatican Greg Burke ameambia wanahabari “papa yuko salama”.
Papa amewahi kuteleza na hata kuanguka mara kadha awali, na kila mara huwa anainuka peke yake au kusaidiwa na mmoja wa wasaidizi wake, shirika la AP linasema.
Kila mara huenda anaendelea na shughuli zake baadaye kama kawaida.

No comments:

Post a Comment