Sunday, 3 July 2016

MAN UNITED MJUENI MHIKITARYAN, MCHEZAJI ATAKAYEBADILISHA MASHAMBULIZI YENU

Kwa habari zilizojitokeza hivi karibuni kwenye mtandao wa Borrusia Dortmund ni kwamba klabu hiyo imekubali dau la Man Utd kwa ajili ya mchezaji wao Henrikh Mkhitaryan na atajiunga na klabu hiyo msimu ujao.Japo Man United wao hawajatangaza rasmi usajili huu ila inaonekana kuwa Mourinho hatimaye kampata mchezaji huyu baada ya kutumu dau jipya la Euro million 30, kwani dau lao la kwanza lilikataliwa. Mkataba wa Mkhitaryan ulikuwa unategemea kuisha msimu ujao na Dortmund hawakuwa na budi kumuuza kwa sababu wangempoteza bure msimu ujao.

Mchezaji huyu wa ki Armenia mwenye miaka 27 anaweza kufanya kila kitu kule mbele akitumiwa vizuri na klabu hii na licha ya dau lilochukua kumsajili, anaweza kuwa kati ya usajili wenu bora mliowahi kufanya kwa miaka mingi.
Mchezaji huyu mwenye miaka 27 alijatambulisha kwa dunia kwa mara ya kwanza alipokuwa akichezea Shakhtar Donetsk kuanzia mwaka 2010-2013, hii ni klabu ile ile walipotokea nyota wengine kama Douglas Costa na Alex Texeira. Miaka hiyo alikuwa kati ya wachezaji muhimu zaidi walioisaidia klabu hiyo kutwaa ubingwa wa ligi ya Ukraine kwa misimu mitatu mfululizo. Alichaguliwa kuwa mchezaji wao bora mwaka 2012 na mwaka 2013 alimaliza kama mfungaji bora wa ligi hiyo.
Kipaji alichonesha Mkhitaryan kiliweza kuonekana na kocha wa Dortmund kwa wakati huo Jurgen Klopp na alikubali kumsajili kwa kiasi cha Euro million 27.5 miaka mitatu iliyopita ikiwa ni dau kubwa kabisa ambalo klabu ya Dortmund iliwahi kutumia kusajili mchezaji. Miaka yake ya kwanza lakini kwenye klabu ya Dortmund haikuridhisha sana na alishindwa kurejesha ile ‘form’ yake iliyomwezesha kunga’aa Donetsk.
Akiongea na mtandao wa fourfourtwo mapema mwaka huu Mkhitaryan alisema kuwa dau lake kubwa lilikuwa kama mzigo kwake lakini Klopp alijitahidi kumsaidia na swala hilo .”Ni kweli Klopp alinisaidia sana kwenye hili sual, aliniambia kwamba dau la usajili si jambo linalohusiana na kitu anachotaka mchezaji na ni suala baina ya klabu mbili tu, nikagundua kwamba yuko sawa na nikasahau masuala  ya pesa.”
Lakini Mkhitaryan hakuweza kuonesha uwezo wake wote mpaka pale Klopp alipotimka na Tomas Tuchel kuchukua virago vyake Signal Iduna Park.
Chini ya Tuchel msimu uliopita Dortmund walirudi tena kwenye ubora wao baada ya kumaliza nafasi ya 7 katika msimu wa mwisho wa Klopp na wakaweza kukogombania ubingwa wa Bundesliga kwa mara nyingine tena.Licha ya kuwa walimaliza nyuma kabisa ya bingwa Bayern Munich, pointi 78 walizokusanya Dortmund msimu uliopita zingewawezesha kutwaa ubingwa wa ligi hiyo kwenye misimu yote kasoro minne kwenye historia ya Bundesliga.
Tuchel aligundua mchezaji aliyekuwa nae kwa Mkhitaryan na akabadilisha mbinu zake ili kumwezesha Mkhitaryan kuonesha uwezo wake wote.
Fundi huyu kwa kawaida alikuwa akiwekwa winga ya kulia kwenye mfumo wa 4-3-3 huku Marco Reus akichukua upande wa kushoto na Aubemayang akiwa mshambuliaji, nyuma yao walikaa Julius Weigl kinda mwenye miaka 20 na Ilkay Gundogan jembe jipya la Man City.
Nyuma ya Mkhitaryan kwenye upande wa kulia wa uwanja walikuwa mmoja kati ya Shinji Kagawa, Gonzalo Castro na Christian Pulisic ambao kucheza kwao kulitegemea maagizo ya kocha kwa mechi hiyo.
Kwa mara nyingi mchezaji aliyekuwa upande wa kulia alipewa maagizo ya kutanua sana upande huo wa uwanja na wakati huo huo kumsaidia beki wa kulia. Jambo hili lilimpa Mkhitaryan uhuru wa kucheza popote pale anapotaka, akicheza nafasi yeyote ile anayotaka kule mbele ambapo anaweza kuleta madhara zaidi
Swala hili lilimaanisha kuwa licha ya nafasi yake aliyoanza upande wa kulia. Mkhitaryan alijikuta akicheza katikati zaidi kama No 10 wa timu. Jambo hili lilimsaidia Mkhitaryan kufunga magoli 18 na kupata ‘assist’ 20 msimu uliopita kwenye makombe yote.
Uwezo wa Mkhitaryan kucheza nafasi nyingi uwanjani hakika utamfurahisha Jose Mourinho ambaye anapendelea mfumo wa 4-2-3-1 na ambaye miaka hii ya karibuni amependelea kuchezesha viungo watatu wanaoweza kucheza nafasi mbalimbali nyuma ya mshambuliaji mmoja tegemezi.
Moja ya matatizo ya Man United msimu uliopita ni mfumo wao kuonekana kama kisu butu kwenye mechi na mchezaji kama Mkhitaryan anaweza kutatua tatizo hilo.
Tangu alipokuwa Inter Milan, Mourinho upendelea kumchezesha No 10 hatari kama Wesley Sneijder alipokuwa Inter Milan na Mesut Ozil Real Madrid.Man United wanajulikana kwa kushambulia sana na ma winga na miaka hii ya karibuni wameshindwa kupata mchezaji aliyengaa nafasi ya No 10, Kagawa alisajiliwa ili kutatua tatizo hili bila mafanikio lakini usajili huu wa Mkhitaryan unaashiria kwamba Mourinho atachezesha mfumo wake anaoupenda na ataachana na ule wa Man United uliozoeleka.
Pia usajili huu unaashiria kwamba inawezekana kuwa kwa mara nyingine kama ilivyokuwa kwenye klabu ya Chelsea alipotua Mourinho, mda wa Juan Mata Man Utd umekwisha.
Mkhitaryan si mchezaji wa kawaida kama ilivyozoeleka kwani jamaa huyu anaongea lugha 6 na pia ana degree ya Uchumi, Mkhitaryan anasema kuwa anapenda kutumia akili yake kwenye mpira “Nacheza mpira kama navyocheza mchezo wa Chess.” Mkhitaryan aliwaambia waandishi wa habari 2013.”Unabidi ufikirie sana nini kinaweza kutokea baada ya kufanya kitu kwenye mchezo.”
“Ukifanya kosa mpinzani wako anaweza kukuadhibu na mwishowe unapoteza hiyo mechi.” Aliendelea .”Sehemu hatari zaidi ni katikati ambapo ni lazima upashambulie au upalinde kama na ni hivyohivyo kwenye mchezo wa Chess.”
Kwa Mkhitaryan Man United wameweza kusajili mmoja wa viungo washambuliaji bora zaidi duniani aliyekuwa kwenye ubora wake sasa hivi na hakika wanasubiri kwa hamu kuona uwezo wake akicheza nyuma ya Zlatan Ibrahimovic msimu ujao.

No comments:

Post a Comment