Sunday, 24 July 2016

Kauli ya CHADEMA baada ya wanachama wake kutangaza kujiunga CCM

Wakati wa Mkutano Mkuu wa CCM jana mjini Dodoma, Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA) kiliwapoteza wanachama wake watatu baada ya kutangaza rasmi kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Wanachama hao waliokihama chama hicho ni Fred Mpendazoe ambaye alikuwa mwanachama wa CCM pia aliwahi kuwa Mbunge wa Kishapu mwaka 2005 hadi 2010 kupitia CCM, Mgana Msindai aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida na mbunge wa zamani wa Iramba Mashariki na mwigizaji wa filamu nchini Tanzania Jackline Wolper.

Mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA alipohojiwa jana wakati kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kinaendelea alisema kuwa, hawana muda wa kukaa na kuanza kumjadili mtu mmoja mmoja anayesemekana kuhama chama hicho.

"Kamati Kuu ni kikao kizito sana, hatuwezi kuacha kujadili masuala ya msingi na kuanza kuwajadili hao wanaosemekana kuwa wamehama chama," alisema mjumbe huyo.

Kamati Kuu ya CHADEMA imekutana jana na leo katika vikao vya dharura ikiwa na lengo kubwa la kujadili mwenendo wa hali ya kisiasa nchini.

No comments:

Post a Comment