MAMLAKA
ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) hatimaye wametaja mfanyabiashara ambaye
alibainishwa na Rais John Magufuli katika hafla ya kuwaapisha Wakuu wa
Mikoa na Wilaya, Ikulu Dar es Salaam juzi.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU,
Valentino Mlowola alimtaja mfanyabiashara huyo kuwa ni Mohammed Mustafa Yusuf Ali anayetuhumiwa
kuiibia Serikali matrilioni ya shilingi kwa kutumia mashine za
kielektroniki (EFDs) ambazo hazijasajiliwa na TRA na kutoa risiti
bandia.
Alisema
TRA kwa kushirikiana na TAKUKURU inaendelea na uchunguzi ili kubaini
makampuni yote yanayojihusisha na udanganyifu huu, ambapo hadi sasa
jumla ya makampuni manne yamebainika kujihusisha na ukwepaji kodi kwa
mtindo huu kuanzia mwaka 2010 hadi 2014; na jumla ya Sh 29,216,900,301.7
imebainika kutokulipwa serikalini na makampuni hayo kwa kipindi hicho.
Alisema
kwa sasa wanaendelea na mahojiano naye zaidi ili kuwabaini wote
wanaohusika na mfumo huo na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Kwa
mujibu wa Kamishna Mkuu wa TRA, Alfayo Kidata aliyeambatana na Mlowola
katika mkutano huo wa waandishi wa habari, makampuni hayo yamekuwa
yakinunua risiti za manunuzi bandia kutoka kwa watu wanaomiliki mashine
za EFDs ambazo hazijasajiliwa.
“Makampuni
hayo wakishanunua risiti za manunuzi bandia, hatimaye huzitumia risiti
hizo kudai marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) bila kuwepo na
bidhaa au huduma halisi iliyouzwa au kutolewa na mhusika, kitendo
ambacho kinainyima serikali mapato stahiki kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Aliyataja
makampuni hayo kuwa ni pamoja na Skol Building Material Ltd ambayo
tangu mwaka 2012 hadi 2013 haikulipa jumla ya VAT ya Sh 5,464,915,963 na
Kodi ya Mapato yenye thamani ya Sh 10,960,787,861 ambayo jumla ya kodi
inayodaiwa ni Sh 16,425,703,824 kwa kipindi hicho.
Kampuni
nyingine ni Farm Plant (T) Limited ambayo tangu mwaka 2010 hadi 2014
haikulipa jumla ya VAT ya Sh 5,930,170,573 na kodi ya mapato yenye
thamani ya Sh 4,948,393,516 ambayo jumla ya kodi inayodaiwa ni Sh
10,878,564,089.
Pia
imo kampuni ya A.M.Steel & Iron Mills Limited ambayo kuanzia mwaka
2013 hadi 2014 haikulipa jumla ya VAT ya Sh 79,016,112 na kodi ya mapato
yenye thamani ya Sh 131,693,518 ambayo jumla ya kodi inayodaiwa ni Sh
210,709,630.
Kampuni
nyingine ni A.M Trailer Manufacturers Limited ambayo tangu mwaka 2013
hadi 2014 haikulipa VAT ya Sh 638,221,034.80 na kodi ya mapato yenye
thamani ya Sh 1,063,701,724. 00 ambayo jumla ya kodi inayodaiwa ni Sh
1,701,922,758.00.
Alisema
baada ya kubaini ukwepaji kodi huo kwa kushirikiana na TAKUKURU
inaendelea na uchunguzi wa tuhuma hizo na mara baada ya uchunguzi
kukamilika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika
kukwepa kodi.
No comments:
Post a Comment