SERIKALI
za mikoa ya Kilimanjaro na Manyara zimelifunga Bwawa la Nyumba ya Mungu
kwa kipindi cha mwaka mmoja ili kuepusha kutoweka kwa viumbe hai
wakiwamo samaki kutokana na kushamiri kwa uvuvi haramu.
Aidha,
wakuu wa wilaya za Moshi, Mwanga na Simanjiro wametakiwa kusimamia
maamuzi hayo na kuchukua hatua kali za kisheria kwa watakaokaidi agizo
hilo.
Mkuu
wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Mecky Sadiki alisema hayo wakati wa hafla
maalumu ya kuwaapisha wakuu wapya wa wilaya mkoani Kilimanjaro
iliyofanyika mjini Moshi, juzi.
Alisema
uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha ujirani mwema baina ya mikoa hiyo
kupitia wilaya tatu zinazolizunguka bwawa hilo na kwamba utekelezaji wa
agizo hilo umeanza rasmi Julai Mosi mwaka huu.
“Hali
ya uvuvi haramu katika Bwawa la Nyumba ya Mungu ni mbaya sana,
mazingira yameharibiwa, kuna athari nyingi zinajitokeza ikiwamo ya
kupungua kwa maji katika bwawa hilo na hii huenda ikaathiri uzalishaji
umeme na kutoweka kwa viumbe hai....kama serikali hatuwezi kuvumilia
tena,” alisema Sadiki.
Pamoja
na bwawa hilo, Sadiki alitaka wakuu wa wilaya kusimamia agizo la Kamati
ya Ushauri ya Mkoa (RCC), kupiga marufuku misumeno ya mnyororo, kwani
imebaini ni adui mkubwa wa misitu.
Katika
hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa aliwakabidhi wakuu hao wa wilaya
migogoro mikubwa mitano iliyopo katika hatua mbalimbali za utatuzi wake
kupitia viongozi waliowatangulia na kutaka kufuata sheria katika
kuishughulikia.
Miongoni
mwa migogoro aliyoitaja ni unaohusisha jamii ya wafugaji wanaozunguka
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kampuni
inayohudumia uwanja huo ya KADCO kuhusu umiliki wa eneo la ardhi.
Mgogoro
mwingine ni wananchi wa wilaya ya Longido mkoani Arusha na mwekezaji wa
eneo la utalii la Ndarakwai uliowahi kusababisha kuchomwa moto kwa eneo
hilo.
No comments:
Post a Comment