Mikel Arteta ameandika barua ya wazi kwa mashabiki wa Arsenal akithibitisha kuondoka klabuni hapo na kujiunga na benchi la ufundi la Manchester City.
Arteta ambaye ni raia wa Uhispania anaenda kujiunga na Pep Guardiola Etihad baada ya kuamua kustaafu rasmi kucheza soka wakati huu akiwa na umri wa miaka 34 baada ya kucheza jumla ya michezo 259 akiwa Everton na Arsenal.
Hata hivyo kwa misimu iliyopita hakuwa na kiwango bora kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara, hali iliyopelekea kucheza jumla ya michezo 26 kwenye misimu miwili.
Akiwa kama mchezaji na nahidha wa Arsenal, Arteta amefanikiwa kubeba makombe mawili ya FA na kufunga magoli 17 kwenye michezo 150 aliyocheza klabuni hapo.
Arteta anaelezea maisha kunako klabu ya Arsenal kama ni yenye thamani na heshima kubwa na hivyo anawatakia kila la heri mashabiki, makocha, viongozi na wachezaji wote wa Arsenal kwa siku ziijazo, huku akitanabaisha kuwa anajisikia mwenye furaha kubwa kuungana na Guardiola.
Maelezo yote ya barua yake haya hapa
Ndugu wapendwa,
Kufuatia tetesi nyingi kutoka kwenye vyombo vya habari juu ya mustakabali wangu, sasa naweza kuthibitisha kwamba naondoka Arsenal na kustaafu soka kabisa ili kuanza maisha mapya ya ukocha kwenye klabu ya Manchester City.
Nimekuwa ni mwenye furaha kwa kipindi chote cha miaka mitano niliyokaa Arsenal, na nisiwe mchoyo wa fadhila kutokana na kupewa heshima kubwa kuwa nahidha wa klabu kubwa kama hii.
Ningependa kwa moyo mkunjufu kabisa kumshukuru kocha wangu, bodi, wachezaji wenzangu wote na bila kusahau mashabiki kwa sapoti isyo na kifani niliyopata kwa kipindi chote nilikuwa hapa
Nitaendelea kukumbuka kipndi changu chote nilichodumu hapa kutokana na kupata kumbukumbu nyingi sana na hakika niatadumu nazo milele. Hakuna kikubwa zaidi ya kubeba Kombe la FA mara mbili na Ngao ya Jamii kwa msimu miwili mfululizo. Makombe ambayo klabu iliyapata kwa mara ya kwanza baada ya miaka 10.
Kwenye kipindi chote cha maisha yangu ya soka nimekuwa na bahati kubwa ya kucheza kwenye vilabu bora. Maamuzi ya kuja Uingereza yalikuwa yenye faida kwangu kama mchezaji kutokana na kunufaika ndani ya uwanja na nje ya uwanja kama ambavyo naenda kuwa kwa sasa.
Sitasahau sapoti ambayo nimekuwa nikiipata kutoka kwa mashabiki na watu kwenye klabu zote nilizowahi kucheza hapa Uingereza.
Lazima nitoe shukrani za kipekee kwa heshima kubwa niliyopata kutoka mashabiki wa klabu za Rangers na Everton kwa miaka yote nilidumu humo vile vile sapoti niliyopata kwa mashabiki wa PSG na Real Socieadad bila kusahau klabu yangu ya kwanza kabisa kuanza kucheza soka la ushindani ya Barcelona…Asanteni sana kwa kila kitu.
Kilichobaki kwangu kwa sasa ni kukabiliana na changamoto mpya kuelekea klabu ya Manchester City. Fursa ya kuungana na Pep Guardiola na timu yake ni fursa adhimu kwangu na ama hakika ninayo furaha kubwa kuona mustakabali wangu wa baadaye.
Kwenye maisha yangu yote ya soka, nimekuwa si tu napenda kucheza uwanjani bali pia kusaidia kuendeleza timu nikiwa nje ya uwanja.
Taaluma ya ukocha imekuwa ni kitu ninachokipenda kwa muda mrefu na kuanzia miaka michache iliyopita nilianza kujifunza nikiwa ndani ya uwanja na nje ya uwanja ili kupata ujuzi zaidi na kuufanyia kazi pale nitakapostaafu kucheza soka.
Nimekuwa na bahati kubwa kucheza chini ya makocha na mameneja bora ulimwenguni kwenye maisha yangu yote ya soka na naamini nitatumia vizuri ujuzi wote niliopata kutoka kwao na uzoefu nilionao kutokana na kucheza soka kuisadia klabu ya Manchester City kupata mafanikio.
Asanteni sana kwa mara nyingine tena, naomba sote kwa pamoja tuendelee kuufurahia mchezo huu wa soka.
No comments:
Post a Comment