WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaagiza kutoka nje ya nchi tani
70,000 za sukari ambapo kati ya hizo, tani 11,957 zimeshawasili nchini
na zitaanza kusambazwa kesho (Jumatano).
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Mei 10, 2016) wakati akizungumza na
waandishi wa habari kwenye mkutano uliofanyika nyumbani kwake Oysterbay
jijini Dar es Salaam.
Akitoa
ufafanuzi wa sukari ambayo imekwishawasili nchini, Waziri Mkuu alisema
tani 2,000 zitapelekwa mikoa ya Kaskazini, tani 3,000 (mikoa ya Kanda ya
Ziwa), tani 2,000 (mikoa ya Kusini), tani 2,000 (Nyanda za Juu Kusini)
na tani 2,000 (mikoa ya Kanda ya Kati).
“Tani
nyingine 24,000 za sukari zitawasili Ijumaa hii na hadi zitoke
bandarini itakuwa kama Jumapili kwa hiyo zinaweza kusambazwa kuanzia
Jumatatu. Tani nyingine 20,000 zitawasili baadaye, ama mwishoni mwa
mwezi huu au mapema mwezi Juni,” alisema Waziri Mkuu.
Amesema anawataka Watanzania wasihofu kuhusu uhaba wa sukari uliojitokeza hivi karibuni kwani umesababishwa na watu wachache.
“Mheshimiwa
Rais ameagiza watu waliohodhi bidhaa hii wakamatwe na sukari isambazwe.
Lakini pia tunaagiza kwa muda mfupi kwa sababu viwanda vyetu
vinatarajia kuanza uzalishaji ifikapo Julai,” alisema.
Amewataka wasambazaji wa sukari waziuze kwa wafanyabishara wadogo ili wao wawawuzie wananchi kwa bei elekezi ya sh. 1,800.
Pia
amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanasimamia
zoezi la ukaguzi ili kubaini zaidi wale waliohodhi bidhaa hiyo.
Akifafanua
kuhusu mkakati wa Serikali kuongeza uzalishaji wa sukari nchini, Waziri
Mkuu amesema nia ya Serikali ni kuhakikisha tatizo la uhaba wa sukari
nchini linakwisha ifikapo 2019.
“Wananchi wasiogope, Serikali imechukua hatua kwa udhibiti mzuri ili tusije kuporomosha soko letu la ndani,” alisema.
“Tunao
mkakati wa kuboresha viwanda vya ndani, wenye viwanda wenyewe au kwa
ubia na wawekezaji kutoka nje, wanaweza kufungua mashamba kwenye maeneo
matatu tuliyotenga kwa ajili hiyo,” alisema.
“Serikali
imetenga maeneo matatu yanayofaa kwa kilimo cha miwa huko Bagamoyo,
Ngerengere na Kigoma. Huko wanaweza kulima na kujenga viwanda vya sukari
na uzalishaji ukawa unapanda mwaka kwa mwaka hadi tutakapoweza
kuimaliza hii gap iliyopo,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI,
S . L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMANNE, MEI 10, 2016
No comments:
Post a Comment