Kwa mujibu wa taarifa ya uokoaji na athari za mafuriko iliyotolewa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa huu, Amina Masenza kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene, shughuli za uokoaji zinaendelea licha ya mazingira kuwa magumu kutokana na maeneo mengi yaliyozingirwa na maji kutofikika kirahisi.
Kwa mujbu wa Masenza, walichokizingatia zaidi ni kuhakikisha watu hawafi kutokana na maji wala kwa kukosa huduma muhimu, ndio maana hatua mbalimbali za kuwaokoa zilianza kuchukuliwa mapema kabla na hata baada ya mafuriko hayo kutokea.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi, sehemu ya Mipango na Uratibu mkoani humu, Nuhu Mwasumilwe alimweleza Waziri huyo kuwa waliomba helikopta mbili kwa ajili ya kufika kwenye maeneo yaliyozingirwa na maji kufanya tathmini ya athari za mafuriko, ikiwa ni njia mojawapo ya kujua ukubwa wa tatizo katika maeneo yasiyofikika kwa njia za kawaida kutokana na maji.
Alitaja hatua mbalimbali zilizochukuliwa na mkoa kuhakikisha watu wanaokolewa kuwa ni pamoja na kuanzisha kambi za muda kwa ajili ya waathirika wa mafuriko katika kijiji cha Kisanga na Itunundu.
“Hatua nyingine ni kuwahudumia waathirika hao kwa kuwapa mahitaji muhimu ikiwemo chakula, matibabu na vifaa vingine kama vile magodoro na mablanketi kutoka kwa wadau mbalimbali waliowachangia,”alisema.
No comments:
Post a Comment