Aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amemtaka Rais John Magufuli atangaze mshahara na marupurupu yake, kwa kuwa amejivisha joho la kuwa Rais wa wanyonge.
Profesa Lipumba amelieleza gazeti la Mwananchi kuwa Rais
Magufuli amejipambanua kuwa kiongozi anayeguswa na matatizo ya wanyonge,
hapendi makuu, anahimiza ukusanyaji wa mapato ya Serikali na matumizi
mazuri ya fedha za umma, lakini watanzania hawajui mshahara wake ni kiasi gani
Profesa
huyo aliyejikita katika masuala ya uchumi, alirejea mijadala mbalimbali
iliyowahi kuibuliwa kuhusu mshahara wa Rais, ikiwamo ule uliyowahi
kuibuliwa mwaka 2013 na Zitto Kabwe, wakati huo akiwa Naibu Katibu Mkuu
wa Chadema kuwa Rais analipwa Sh32 milioni kwa mwezi.
Pia
alirejea taarifa iliyochapishwa na Mwananchi, Julai 27, 2015,
iliyoandikwa kutoka katika mtandao wa African Review kuwa Rais mstaafu
Jakaya Kikwete ni wa nne miongoni mwa marais wa Afrika kwa kupata
mshahara mkubwa wa dola za Marekani 192,000 kwa mwaka sawa na dola
16,000 kwa mwezi, ambayo ni sawa na Sh32 milioni kwa mwezi. Hadi jana
jioni, dola moja ya Marekani ilikuwa sawa na Sh2,187.
“Taarifa
ya Ikulu ilikanusha vikali habari zilizochapishwa na Mwananchi. Ikulu
ilieleza kuwa habari hizo siyo za kweli. Hata hivyo, haikueleza mshahara
wa Rais na marupurupu yake ni kiasi gani?
Pia, katika mjadala
wa mshahara wa Rais, Naibu Spika wa Bunge lililopita ambaye ndiye Spika
wa sasa, Job Ndugai alinukuliwa akieleza kuwa mshahara wa mtu ni siri
yake.
Waziri wa Nchi Katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
utumishi wa Umma wa wakati huo, Celina Kombani (kwa sasa ni marehemu)
alisema kuwa ni kosa kutangaza mshahara wa Rais.
“…Kwa hivi sasa
Rais Magufuli atangaze mshahara na marupurupu yake na kama mapato yake
ni Sh32 milioni kwa mwezi, basi ajitolee alau nusu ya mapato hayo
kuchangia elimu na afya ya wanyonge. Hatua hii itaimarisha taswira
inayojengeka barani Afrika kuwa yeye ni Rais wa wanyonge,” amesema
Lipumba.
Wakati akizungumza na wazee wa Dar es Salaam wiki
iliyopita, Rais Magufuli aliwataka mawaziri, naibu mawaziri na makatibu
wakuu wachangie Sh1 milioni katika mishahara yao kuchangia elimu.
Pia
Rais alieleza kuwa yeye mwenyewe, makamu wake na waziri mkuu
watachangia Sh6 milioni kila mmoja, ili zifike Sh100 milioni kusaidia
changamoto za elimu bure Mkoa wa Dar es Salaam.
Kutokana na
tangazo hilo, Profesa Lipumba alisema, “Ikiwa Sh6 milioni zitakatwa
katika mshahara wake wa mwezi mmoja ni wazi mshahara wake na ule wa
makamu wake na waziri mkuu ni zaidi ya Sh6 milioni kwa mwezi.
“Mishahara
na marupurupu ya viongozi wa Tanzania hayako wazi. Watanzania hawajui
kila mwezi Rais, Makamu wa Rais na viongozi wakuu wa Serikali wanalipwa
kiasi gani? Malipo ya wabunge pia hayako wazi?” alihoji.
Profesa
Lipumba ambaye amewahi kuwa msaidizi wa Rais katika masuala ya uchumi
kati ya mwaka 1991 na 1993, alisema kwa kuwa Rais Magufuli amejivisha
joho la kuwa Rais wa wanyonge, anawajibika kuwaeleza Watanzania mshahara
na marupurupu yake.
“Ikiwa mshahara ni mkubwa sana achukue hatua za kuupunguza kama alivyofanya Mwalimu Nyerere mwaka 1965.”
Hata
hivyo, alisema kifungu cha Katiba cha 43 (2) kinaeleza kuwa mshahara na
malipo mengineyo yote ya Rais havitapunguzwa wakati Rais atakapokuwa
bado ameshika madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba.
Profesa Lipumba alisema Rais Magufuli akitaka kupunguza mshahara wake itabidi kwanza abadilishe kifungu hicho cha Katiba.
“Anaweza kujitolea mchango wa kudumu utakaokatwa kutoka kwenye mshahara wake kusaidia sekta ya afya au elimu,”alisema.
Profesa
Lipumba ambaye ni mshauri wa Benki ya Dunia (WB) na Benki Kuu ya
Tanzania (BoT) katika masuala ya uchumi, alisema ili kuimarisha utawala
bora ni muhimu uongozi ulio madarakani utumie mamlaka waliopewa kwa
manufaa ya Taifa.
“Mishahara na marupurupu ya viongozi yawe wazi
na yaamuliwe na kupangwa na taasisi iliyo huru. Kuweka utaratibu ulio
wazi wa kuamua mishahara na marupurupu ya viongozi wa umma wakiwamo Rais
na makamu wake, mawaziri, wabunge, majaji, makatibu wakuu na viongozi
wengine,”alisema.
Alisema ni muhimu katika ujenzi wa utawala bora, uwajibikaji na uwazi wa viongozi wa umma kwa wananchi wanao waongoza.
“
Inasemekana mshahara wa mbunge katika Bunge lililopita ulikuwa Sh3.4
milioni kila mwezi.Pia mbunge alilipwa Sh8.2 milioni, nyingine kama
posho ya jimbo, gharama za ofisi, mafuta, malipo ya wasaidizi wake na
dereva.
“Vile
Vile, mbunge anapohudhuria kikao cha Bunge alilipwa posho ya Sh80,000
za kujikimu, Sh50,000 za mafuta ya gari na Sh200,00 za kuhudhuria kikao
cha Bunge, jumla ni Sh330,000 kwa siku.
“Posho ya siku moja ya
mbunge ni zaidi ya mara mbili ya kima cha chini cha mshahara wa Serikali
kwa mwezi mzima ambacho ni Sh150,000. Mishahara inakatwa kodi,
marupurupu hayakatwi kodi,”alisema.
No comments:
Post a Comment