Saturday, 5 December 2015

Siku 7 za wakwepa kodi kaa la moto

Katika agizo hilo la juzi, Dk Magufuli alisema muda huo ukipita, Serikali itachukua hatua za kisheria dhidi ya wafanyabiashara hao, walioondoa makontena bandarini bila kulipa kodi. Akizungumza jana na waandishi wa habari, Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kodi (TRA), Dk Philip Mpango, alisema tayari baadhi ya kampuni za wafanyabiashara hao, zimeanza kulipa kodi husika, huku akibainisha kuwa makontena hayo 329, yote yaliondolewa bila kulipa kodi katika Bandari Kavu inayomilikiwa na mfanyabiashara Said Salim Bakhresa.
Majina Dk Mpango alitaja kampuni zilizokwepa kodi hiyo kuwa ni pamoja na Lotai Steel Tanzania LTD, iliyokuwa na makontena 100; Tuff Tyres Center Company, iliyokuwa na makontena 58 na Binslum Tyres Company, iliyokuwa na makontena 33. Kampuni nyingine ni Tifo Global Mart (Tanzania) Company Limited, iliyokuwa na makontena 30; IPS Roofing Company Limited, iliyokuwa na makontena 20, Rushywheel Tyre Center Co Ltd, iliyokuwa na makontena 12.
Pia ipo kampuni ya Kiungani Trading Co Ltd, iliyokuwa na makontena 10; Homin International Limited, iliyokuwa na makontena tisa; Red East Building Material Company Limited, makontena saba; Tybat Trading Co Limited, makontena matano; Zing Ent Ltd, mkontena manne na Juma Kassem Abdul, makontena matatu.
Wengine ni Salum Link Tyres, makontena matatu; Ally Masoud Dama, makontena mawili; Cla Tokyo Limited, makontena mawili; Farid Abdullah Salem, makontena mawili; Salum Continental Co, makontena mawili; Zuleha Abbas Ali, makontena mawili; Issa Ali Salim, makontena mawili na Snow Leopard Building, makontena mawili.
Kampuni na wafanyabiashara waliokuwa na kontena moja moja ni Abdulaazizi Mohamed Ally; Ahmed Saleh Tawred; Ali Amer; Ally Aweza Alhamdany; Awadhi Salim Saleh; Fahed Abdallah Said; Hani Said; Hassan Hussein Suleyman; Humud Suleiman Humud; Kamil Hussein Ali; Libas Fashion; Nassiri Salehe Mazrui na Ngiloi Ulomi Enterprises Ltd.
Wengine wenye kontena moja ni Omar Hussein Badawy; Said Ahmad Hamdan; Said Ahmed Said; Salumu Peculier Tyres; Sapato N.Kyando; Simbo Yohan Kimaro; Strauss International Co Ltd na Saleh Mohamed Saleh.
Dk Mpango alisema bidhaa zilizokuwemo katika makontena hayo ni matairi ya magari yenye samani mbalimbali, betri za magari, vifaa vya ujenzi, nguo na bidhaa nyingine mchanganyiko.
Waliojitokeza Alisema wahusika wameshaanza kujitokeza kulipa sehemu ya kodi wanazodaiwa na tayari wamepokea Sh bilioni 5.23 kutoka kwa Said Salim Bakhressa and Company Limited, Sh bilioni 2.17 Novemba 20 mwaka huu, Tuff Tyres Center Sh bilioni moja Desemba 2 mwaka huu; Binslum Tyres Co Ltd Sh bilioni 1.4 alizolipa Desemba 2 mwaka huu na Sh bilioni 1.15 alizolipa juzi.
Wengine waliolipa ni Kiungani Trding Co Ltd Sh milioni 506.7 Desemba 2, mwaka huu, zote zikiwa kodi iliyokadiriwa na jana mchana Bakhressa walimtarajia kulipa Sh bilioni 2 za nyongeza.
Leseni za ICD, mawakala Dk Mpango alisema TRA inapitia upya taratibu za utoaji leseni za bandari kavu, ili kuondoa mianya na kuweka udhibiti katika uondoshaji wa mizigo katika bandari zote kavu na bohari za forodha.
“Sambamba na hatua hizi, TRA inafuatilia kwa kina kubaini mawakala wote wa forodha walioshiriki katika upotevu wa makontena na kuwachukulia hatua, ikiwemo kuwafungia leseni pamoja na adhabu nyingine kwa mujibu wa sheria,“ alisema Kamishna Mpango.
Alisisitiza kuwa wote waliohusika na uondoshwaji wa makontena kutoka badari kavu kinyume cha taratibu, wajitokeze kwa hiari kulipa kodi yote wanayodaiwa kabla muda wa siku saba za huruma ya Rais Magufuli haujaisha, kwani zimebaki siku sita.
Akizungumzia ukaguzi wa makontena yaliyokamatwa maeneo ya Mbezi Tangibovu, yaliyokuwa yakimilikiwa na Heritage Empire Company yakitokea katika Bandari Kavu ya PMM iliyopo Vingunguti, alisema yalibainika kuwa mali iliyokuwemo ilisamehewa kodi na ilikuwa sawa na maelezo kwenye kadhia za forodha.
Hata hivyo, alisema kulibainika kasoro kadhaa kuwa tozo alizolipa mwekezaji ni pungufu ya Sh milioni 58.47 ikiwa ni pamoja na ada ya mchakato wa forodha, Sh milioni 3.66, tozo ya kuendeleza reli Sh milioni 8.2 na kodi ya pango ya forodha Sh milioni 46.6.
Alisema kwa mujibu wa sheria, mizigo ya EPZ hairuhusiwi kukaa kwenye bohari yoyote isiyo chini ya uangalizi wa Kamishna wa Forodha bila idhini wala kibali cha Kamishna ; na kitendo cha kuondoa mizigo kutoka bandari kavu kwenda uraiani ni kinyume cha taratibu za kiforodha.

No comments:

Post a Comment