Thursday, 29 October 2015

Utata waibuka kufutwa matokeo urais Zanzibar.

Hatua ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) kuamua kufuta matokeo yote ya uchaguzi wa Zanzibar kwa madai kumefanyika vitendo vya udanganyifu ikiwamo kura nyingi kuonekana zimepigwa tofauti na orodha ya wapigakura waliosajiliwa katika baadhi ya majimbo kisiwani Pemba, imezua utata.
 
Uamuzi wa kufuta uchaguzi huo ulitangazwa jana majira ya saa 7.45 mchana na Mwenyekiti wa Zec, Jecha Salim Jecha, ambaye alizungumza na waandishi maalum katika ofisi ya tume hiyo iliyopo Maisara na baadaye taarifa hizo kutangazwa na Kituo cha Televisheni cha Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC).
 
Jecha alisema vikwazo vilivyojitokeza katika uchaguzi huo ndivyo vilivyochelewesha utoaji wa matokeo ya uchaguzi ndani ya wakati uliopangwa kisheria na kwamba ndicho kilichoifanya Zec kuamua kufuta matokeo yote ya uchaguzi katika majimbo 54 ya Zanzibar.
 
Alisema kuna sababu tisa zilizosababisha kufikia uwamuzi huo ikiwamo wajumbe ndani ya tume kufikia hatua ya baadhi yao kuvua mashati na kuanza kupigana na wengine badala ya kuwa makamishna wa tume walikuwa ni wawakilishi wa vyama vyao wakati kuna vyama vingi vilivyoshiriki uchaguzi huo, ambavyo havikupata fursa ya kuwa na makamishna ndani ya tume na vinashiriki uchaguzi mkuu.
 
“Kumegundulika kasoro nyingi katika uchaguzi huu miongoni mwa hizo, kubainika kwa baadhi ya vituo hasa Pemba vimekuwa na kura nyingi kuliko Daftari la Wapigakura,” alisema mwenyekiti huyo.
 
Aidha, alisema wamepokea taarifa kutoka kisiwani Pemba kuwa kulifanyika uhamishaji wa masanduku ya kura na kuhesabiwa eneo la nje ya vituo kitendo ambacho ni kinyume cha taratibu za sheria za uchaguzi, pamoja na mawakala wa Chama cha Tadea kutolewa nje ya vituo wakati zoezi la upigaji kura likifanyika katika majimbo mbalimbali kisiwani Pemba.
 
Mwenyekiti huyo alisema Zec imeridhika kuwa kuna vituo vilivamiwa na vijana kuonekana kuandaliwa na vyama vya siasa na kufanya fujo ikiwamo kupiga watu na kuzuiwa watu kufika katika vituo vya kupigia kura kutimiza haki yao ya kikatiba.
 
“Vyama vya siasa vimeonekana kuingilia majukumu ya tume ikiwamo kujitangazia ushindi na kusababisha mashinikizo kwa tume, na kumekuwapo na malalamiko mengi yanayoashiria kutoridhika na mchakato mzima wa upigaji kura, kuhesabu na kutoa matokeo ya uchaguzi huo,” alisema Jecha.
 
Aidha, alisema kuna fomu za matokeo ya vituo vingi vya Pemba namba zake zimefutwa na kuandikwa upya  juu yake, kitendo ambacho kinaonesha kulikuwa na lengo la kufanya udang’anyifu kwa matokeo yaliojazwa katika fomu hizo.
 
“Kwa kuzingatia hayo na mengine, sijayaeleza mimi nikiwa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Zanzibar, nimerizika kwamba uchaguzi huu haukuwa na haki na kunaukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za uchaguzi, hivyo kwa uwezo nilionao natangaza rasmi matokeo yote yamefutwa na kunahaja ya kurudia uchaguzi huu,”alisema.
 
Wakati mwenyekiti huyo akitoa maamuzi hayo makamishna wawili wa tume ya uchaguzi kutoka Chama cha Wananchi (CUF), Nassor Khamis Mohammed na Ayoub Bakari Hamad, wamemtaka rais wa Zanzibar aunde tume ya majaji ya kumchunguza mwenyekiti wa tume hiyo kwa sababu ameshindwa kutekeleza kazi yake aliyopewa kwa kuzingatia katiba na sheria.
Alisema tume hiyo iwapo itathibitika mwenyekiti huyo ameshindwa kufanya kazi, achukuliwe hatua ikiwamo kuondoshwa katika wadhifa huo kwa vile kitendo alichofanya cha kutangaza maamuzi hayo bila ya kuishirikisha tume ni uvunjaji mkubwa wa sheria wa tume ya uchaguzi ambayo inatakiwa itoe maamuzi baada ya kushauriana na akidi ya wajumbe ya kutoa maamuzi iwe imekamilika.
 
“Mwenyekiti kafuta matokeo bila ya kuwapo majadiliano hayo ni maamuzi yake binafsi na sio maamuzi ya tume, hatujawahi kujadili na kupitisha uamuzi kama huo tangu wananchi wakamilishe kazi ya kupiga kura,”alisema Ayoub. 
 
Kamishna Zec aipinga
Bakari Hamad kamishna wa tume hiyo, alisema kwa mujibu wa matokeo yote yaliokusanywa, yanaonesha hakukuwa na tatizo la malalamiko kuhusu mchakato wa uchaguzi ulivyokuwa kwa sababu hakuna fomu za malalamiko zilizojazwa na kuwasilishwa tume kuanzia ngazi ya udiwani, uwakilishi na nafasi ya urais wa Zanzibar. 
 
Ayoub alisema hoja ya kutaka uchaguzi uhairishwe ilianza kujitokeza Oktoba 26, mwaka huu baada ya viongozi wa CCM kuwasilisha malalamiko yao na kutaka uchaguzi huo utangazwe ni batili na urejewe upya bila ya   kuonesha   vielelezo   vya   kuharibika   kwa   uchaguzi    huo. 
 
Alisema waangalizi wa ndani na nje wakiwamo mawakala, wameridhishwa na uchaguzi ulivyokwenda na mpaka juzi majimbo 31 yalikuwa yametangazwa na kazi ya kukamilisha uhakiki wa majimbo 23 ulikuwa ukifanyika wakati mwenyekiti akitoa uwamuzi huo wao makamishna walikuwa wakiendelea kuhakiki matokeo ya uchaguzi huo. Wakizungumza kwa nyakati tofauti makamishna hao, walisema wameshtushwa na mwenyekiti wa tume hiyo kufanya maamuzi yake binafsi na kueleza uamuzi huo hawautambui na kumtaka arejee kazini wakamilishe kazi iliyobakia na kumtangaza mshindi wa uchaguzi huo.
 
Kuhusu nafasi ya urais baada ya uchaguzi huo kufutwa, Ayoub alisema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, “rais ataendelea kuwa rais mpaka rais anayechaguliwa na kuapishwa, utaratibu huo unapokamilisha,” alisema Ayoub.
 
Makamishna hao walikanusha hoja ya mwenyekiti juu ya kuwapo baadhi ya makamishna waliovua mashati na kupigana kwa kutetea misimamo ya vyama vyao na kusahau wajibu wao katika tume kama ilivyoelezwa katika sababu tisa za kufutwa matokeo hayo.
 
“Hakuna watu waliopigana, Bunge la Kenya wabunge wake hufikia kupigana, ufumbuzi hauwi kulivunja bunge, na chaguzi nyingi zimewahi kutokea duniani na ufumbuzi huwa sio kufuta matokeo ya uchaguzi bali kurekebisha kasoro,” alisema.
 
WAKILI MAHAKAMU KUU ZANZIBAR AIPINGA ZEC
Nassor Khamis, ambaye ni wakili mkongwe wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, alisema kwa mujibu wa utaratibu wa kisheria uliowekwa, huwezi kupiga kura bila ya kuwamo katika orodha ya wapigakura na kushangaa madai ya kuwapo kwa kura bandia zinazodaiwa kutumika kisiwani Pemba.
 
Alisema uamuzi uliofanywa na mwenyekiti utaleta matatizo makubwa kikatiba kwa vile wapigakura wa Zanzibar ndio hao hao wapigakura wanaochagua mbunge wa Jamhuri ya Muungano na rais na kama kunaudanganyifu lazima uguse mchakato wa uchaguzi huo.
 
“Zanzibar haitakuwa na wabunge wa Jamhuri ya Muungano kwa sababu wao ndio wanaopiga kura kuchagua rais wa Zanzibar, muwakilishi na udiwani, mbunge na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,”alisema.

No comments:

Post a Comment