Mwenyekiti wa
shirikisho la riadha nchini Kenya (AK) ambaye alikuwa amesimamishwa kazi
kwa muda, Isaiah Kiplagat amefariki. Bw Kiplagat, mwenye umri wa miaka
72, alifariki dunia leo Jumatano mjini Nairobi kutokana na kile jamii
yake ilisema ni kuugua saratani ya muda mrefu.
Bw Kiplagat na maafisa wengine wawili wa chama cha AK, David Okeyo na Joseph Kinyua, walisimamishwa kazi na kitengo cha maadili cha shirika la riadha duniani, IAAF mnamo Novemba 2015.
Watatu hao walidaiwa kuhujumu juhudi za kupambana na matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku za kuongezea nguvu miongoni mwa wanariadha.
Pia walishtumiwa kwa madai ya kupunja pesa za ufadhili kutoka kwa kampuni ya kutengenezea vifaa vya michezo ya Nike.
Kiplagat pia alidaiwa kupokea "msaada" wa magari mawili kutoka kwa chama cha riadha nchini Qatar kati ya mwaka wa 2014 na 2015, wakati mji mkuu wa taifa hilo, Doha ulikuwa unapigiwa upato wa kuwa mwenyeji wa mashindano ya riadha duniani mwaka wa 2019.
Hadi wakati wa kifo chake, Kiplagat alikuwa ameongoza chama cha AK kwa zaidi ya miongo mitatu.
No comments:
Post a Comment