Ukisoma Biblia Kutoka Sura ya 14 (sura nzima) utaona jinsi Mungu alivyomtumia Musa kuwatoa wana wa Israeli kutoka utumwani Misri kwenda nchi ya ahadi, ilifika mahali wana wa Israeli wakaanza kumlalamikia Musa kwa nini umetutoa Misri kuja kutuleta (kufia) Jangwani ambako hakuna makaburi (14:12)? Sura hii inaeleza mambo mengi, utaona jinsi Musa alivyopambana na jeshi la Farao mpaka akawavusha wana wa Israeli salama na jeshi la Farao likaangamia baharini.
Kutoka 15 wana wa Israeli sura nzima wanamsifu Musa baada ya kuwavusha salama (wakimwimbia Bwana wimbo). Mungu aliamuwa kumtumia Musa kuwatoa wana wa Israeli utumwani Misri hadi nchi ya Ahadi, Musa peke yake alikuwa anajua nini kitatokea mbele ya safari (alikuwa na maono) lakini wana wa Israeli wao walikuwa hawatambui juhudi kubwa ya Musa. Wana wa Israeli walikuwa wabishi huku hawana kitu na hawana uhakika na kesho.
Nimeona nianze na utangulizi huo wa Musa na wana wa Israeli, huu ni ujumbe kwa wana Simba (Msimbazi). Binafsi simjui Mohamed Dewji zaidi yakumuona kwenye TV na magazetini.
Soka ni mchezo unaopendwa na watu wengi zaidi duniani, pia soka ni biashara ambayo inahitaji fedha nyingi sana kuendesha, huna pesa usitengemee miujiza wala ushirikina, soka ni pesa na hapo furaha ya soka ndiyo utaiona.
Simba toka ameondoka Kassimu Dewji 2004 kama sikosei, haijawahi kuwa na mafanikio tena zaidi ya siasa za soka la Tanzania. Kuna kitu najiuliza Mohamed Dewji amejitokeza kuinunua Simba kwashilingi bilioni 20 za Tanzania, fedha ambazo ni nyingi sana zikipata wasimamizi wazuri (viongozi).
Viongozi wa Simba hawataki kumuuzia Mohamed Dewji kwa sababu ya kelele za wanachama wanaojiita ndiyo wenye timu ilihali mmoja wao hata akiambiwa tu kupelekea wachezaji maji (Uhai) kwenye mazoezi hawezi, Mohamed Dewji alikuwa mtu sahihi kwa wakati huu kuinunua Simba sababu soka ni pesa siyo maneno.
Mashabiki wanataka Simba ya mwaka 2003 hawahitaji kujua nani anaimiliki wao wanataka furaha, wamechoka kuitwa wa matopeni, mchangani, wa hapahapa n.k.
Manchester City iliuzwa kwa waraabu na sasa ni timu inayotisha, mbona waarabu hawakuinunua na kuipeleka uarabuni? Ni kwa sababu ya vipengele vizuri vya kimkataba ambapo hata Simba wangeweza kutafuta watalaam wazuri wakaandika mkataba mzuri ambapo Mohamed Dewji angeiendeleza Simba kama Simba na siyo kuibadili jina. Viongozi Simba jifunzeni kutoka kwa mataifa yaliyoendelea na hii ilikuwa ni neema kwenu kutoka kwenye shida kwenda kwenye raha kama ilivyokuwa kwa wana wa Israeli.
Kuweni na maamuzi magumu kama ya Aden Rage badala ya kusikiliza kelele za wanachama ambao wakiachiwa timu kuendesha hata kwa wiki mmoja siamini kama wataiweza.
Aden Rage aliamua kumuuza Okwi kwenda Etoile du Sahel ya Tunisia bila kujali kelele za wanachama leo hii matunda yake yanaonekana sababu Rage alikuwa anajua anachokifanya, alimuuza Samata kwenda TP Mazembe leo kila mwana Simba anafurahia. Simba ikifanya vizuri sifa zote kwa wana Simba lakini ikifanya vibaya lawama zote kwa viongozi na si wana Simba wote. Naamini angekuwa Range asingeziacha hizi fedha nyingi huku timu ina hali mbaya vile.
TP Mazembe hawa bahatishi sababu ya uwepo wa Moses Katumbi, hakuna njaa njaa pale leo hii mnataka kufanikiwa kwa kuungaunga? kitu ambacho hakipo duniani. Timu zote kubwa zinafanya vizuri sababu ya kuwa na jeuri ya pesa, hakuna muujiza kwenye soka zaidi ya kuwa na pesa.
Wenzenu upande wa pili wametulia toka 2012 sababu kuna mtu anapesa pale ambaye anaiendesha timu na siku zote fedha inaongea wachezaji, makocha wanauhakika na kesho.
Billion 20 kwa kifupi zingeweza kufanya machache yafuatayo:-
- Kujenga uwanja wenu wa Bunju kwa billion 11 ambapo mechi za ndani mngeweza kuzitumia pale, hostel, ofisi na miundombinu yote ya kisasa ingekuwepo.
- Billion 5 mgeweza kujenga kitega uchumi (business center) cha kisasa katikati ya jiji na kuwapangisha watu ambapo mgepata kodi toka kwa wapangaji.
- Billion 5 zingeendesha timu kwa msimu mzima, kusajili wachezaji aina ya Ngoma 5 tu, kulipa mishahara na uendeshaji wa timu kwa umjula bila wasiwasi wowote.
- Timu kubwa na ya vijana zingeweza kukaa kambini pale bila matatizo.
Simba ingekuwa timu inayoendeshwa kisasa, ambapo ingeleta ushindani kwa Yanga na Azam na ligi yetu ingeweza kuvutia wawekezaji kutoka nje. Kwenye mashindano ya kimataifa tungekuwa washindani na siyo wasindikizaji.
Viongozi Simba jifunzeni kutoka kwa nchi zilizoendelea kisoka. Soka ni makombe na si vinginevyo.
No comments:
Post a Comment