Thursday, 16 June 2016

Utafiti: Asilimia 88 ya Wananchi Wanataka Bunge Lirushwe ‘Live’


TAASISI ya Twaweza imetoa matokeo ya utafiti wake, ambapo imebainika kuwa asilimia 79 ya Watanzania wamepinga uamuzi wa Serikali wa kusitisha matangazo ya moja kwa moja (Live ) ya Bunge.

Katika maoni yao, wananchi hao wamedai kuwa ni haki yao ya msingi kufahamu kinachoendelea katika vikao mbalimbali vya Bunge.

Utafiti wa taasisi hiyo umefanywa katika maeneo tofauti ya Tanzania Bara kupitia mpango wake wa Sauti za Wananchi.

Akitoa taarifa ya matokeo ya utafiti huo jana jijini Dar e Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze,  alisema suala hilo limeonekana kutokuungwa mkono na wananchi wengi.

“Asilimia kubwa ya Watanzania wanapinga uamuzi wa Serikali wa kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya Bunge. Suala hili limeonekana kugusa hisia za watu wengi na maamuzi haya ya Serikali yakionekana kutoungwa mkono.

“Katika utafiti huu wananchi nane kati ya 10 wanapinga uamuzi wa hali inayodhihirisha kutoungwa mkono kwa hatua hiyo,” alisema Eiyakuze.

Akizungumzia sababu walizozitoa  wananchi wanaotaka matangazo ya Bunge yarushwe moja kwa moja,  Eiyakuze alisema asilimia 46 walisema yanawafanya waweze kufuatilia utendaji wa wabunge waliowachagua kwa kuwa huko ndio walikowatuma.

“Asilimia 44 wanasema ni muhimu kwa sababu wananchi wanahaki ya kufahamu kinachoendelea bungeni, asilimia 29 wanasema matangazo ya moja kwa moja yalikuwa yanaaminika zaidi kwa watazamaji na wasikilizaji  kuona na kusikia wenyewe kile kinachoendelea tofauti na mfumo wa kurekodi ambapo kuna baadhi ya mambo yanahaririwa.

“Asilimia 16 walidai kuwa inafursa mwananchi kupata taarifa sahihi badala ya kuzisoma kwenye magazeti huku asilimia 16 nyingine wakisema inawasaidia wanachi kufuatilia mijadala ya Bunge kwa wakati”, alisema Eiyakuze.

Pamoja na hali hiyo mkurugenzi huyo alisema katika utafiti huo asilimia 92  ya wananchi walisema kuna umuhimu wa vipindi vya Bunge kurushwa moja kwa moja kupitia Luninga na redio bila kujali gharama zilizoelezwa kuwa ndio chanzo cha kufikia uamuzi huo.

“Asilimia 88 walisema vipindi vya Bunge virushwe ‘Live’ bila kujali gharama ukilinganisha na asilimia 12 ambao waliona ni muhimu suala la bajeti likazingatiwa,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema asilimia 80 wanaona matangazo ya moja kwa moja kutoka bungeni ni muhimu kama yalivyo na asilimia 20 wakisema fedha hizo zitumike kwenye huduma nyinge za jamii.

Akizungumzia suala la vyombo vya habari vya binafsi kuruhusiwa kurusha matangazo hayo,  Eiyakuze alisema wananchi wanaunga mkono vyombo hivyo kuruhusiwa iwapo Serikali imeshindwa kumudu gharama.

Utafiti huo pia umeonesha Watanzinia wanne kati ya kumi wamewahi kuangalia matangazo ya moja kwa moja kupitia Luninga na sita kati ya kumi  wamesikiliza kupitia redio.

Aidha utafiti huo umeonyesha zaidi ya nusu ya wananchi walosema wameangalia au kusikiliza vipindi vya Bunge wamefanya hivyo ndani ya miezi miwili iliyopita.

Hali ilivyokuwa
Januari mwaka huu, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,  Nape Nnauye, alitoa ufafanuzi bungeni kuhusu hatua ya Serikali kusitisha matangazo hayo kupitia Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC).

Miongoni mwa sababu alizozieleza ni pamoja na kuwepo kwa gharama kubwa ya Sh bilioni 4.2 zinazotumika katika uendeshaji wa matangazo hayo ya moja kwa moja kwa mwaka pia watumishi wa serikali kushabikia Bunge badala ya kuendelea na kazi ofisini.

Hatua ya Serikali kusitisha matangazo hayo iliibua mjadala mkubwa bungeni huku Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, (ACT-Wazalendo) akilitaka Bunge kusitisha shughuli zake ili kujadili taarifa hiyo ya Serikali.

Siku chache baadaye kilio hicho cha ukosefu wa fedha za kuonesha matangazo hayo ya moja kwa moja ambacho kimekuwa kikitolewa na serikali, sasa kilipata ufumbuzi.

Hatua hiyo iliyokana na uamuzi wa Mfuko wa Vyombo vya Habari nchini (TMF), kujitokeza hadharani na kueleza kwamba upo tayari kutoa fedha zinazohitajika ili kuhakikisha haki ya Mtanzania kupata habari kupitia TBC haiingiliwi wala kubughudhiwa kwa hoja yoyote.

Endapo Serikali itakubali ombi hilo, wananchi wataendelea kunufaika na vikao vya moja kwa moja vya Bunge tofauti na pendekezo la serikali la kunakili baadhi ya sehemu na kisha kuoneshwa usiku

No comments:

Post a Comment