Eden Hazard na Thomas Vermaelen wamepona majeraha yao, ambayo yalikuwa yakitishia uwepo wao katika mchezo wa leo wa kundi E dhidi ya Italy ‘Azzurri’, utakaochezwa katika uwanja wa Stade des Lumieres au Stade de Lyon uliopo manispaa ya mji wa Lyon.
Hazard ambaye ni nahodha wa kikosi hicho baada ya kukosekana kwa Vincent Kompany, alipata maumivu ya kifundo cha mguu siku ya Ijumaa.
“Sidhani kama amepata majeraha makubwa sana, ni mgongano tu.” alisema kocha wa Ubelgiji Marc Wilmots.
“Thomas Varmaelen amecheza vizuri mpaka siku ya mwisho mazoezini na yupo tayari kwa mchezo wa leo”, Wilmots aliongeza.
Italy kwa upande wao, walikumbwa na jinamizi la majeraha kabla ya michuano hii, hali iliyopelekea kuwakosa wachezaji wao muhimu kama Maco Verratti na Claudio Marchisio.
Kocha Antonio Conte anatarajia kuwapa nafasi kubwa zaidi katika safu ya ushambuliaji nyota wa Southampton Graziano Pelle na mchezaji wa Inter Eder, huku safu yake ya ulinzi akiwategemea Leonardo Bonucci, Andrea Barzagli na Giorgio Chiellini, wote hawa wakimlinda mkongwe atakayekuwa golini Gianluigi Buffon.
“Ni faida kubwa kuwategemea wachezaji wanne kutoka Juventus ambao wamecheza pamoja kwa muda mrefu katika safu ya ulinzi ya timu yao, na bila shaka ndio lengo letu kuu kuifanya safu yetu ya ulinzi kuwa imara”, Conte aliwaambia waandishi
Lakini kama nilivyotanabaisha hapo awali, napenda kila idara icheze kwa umakini, hivyo ni muhimu sana kuwa na balansi katika timu, kuanzia safu ya ulinzi mpaka ushambuliaji”.
Takwimu muhimu.
- Katika michezo mitano ya mwisho waliyokutana wawili hao, imezalisha jumla ya mabao 18, sawa na wastani wa 3.6 kwa mchezo.
- Ubelgiji wamepoteza michezo mitano ya kati ya saba ya mwisho ya michuano ya Ulaya.
- Italy wamekuwa kati ya mataifa manne ambayo hayakufungwa mchezo wowote wakati wa kampeni za kufuzu kuelekea michuano ya mwaka huu (wengine ni Austria, England na Romania).
- Makocha wa timu hizi mbili Wilmots (Ubelgiji) na Conte (Italy) walikuwa katika vikosi vya kwanza katika michuano hii mwaka 2000 wakati timu zao zilipokutana.
No comments:
Post a Comment