Didier Deschamps atakuwa kwenye mtihani mwingine leo kuhakikisha timu yake inashinda dhidi ya Albania ili kujihakikishia tiketi ya kwenda hatua ya mtoano. Mchezo huu wa raundi ya pili wa kundi A, utapigwa kunako dimba la Stade Velodrome majira ya saa 4 usiku.
Ufaransa ilishinda kwa mbinde mchezo wake kwanza dhidi ya Romania, shukrani za dhati ziende kwake Dimitri Payet ambaye alifunga goli la ushindi dakika za majeruhi baada ya kuhamishiwa namba 10, kufuatia kutolewa kwa Paul Pogba na nafasi yake kuchukuliwa na Anthony Martial, ambaye alienda pembeni alipokuwa akicheza Payet.
Hakuna matarajio yoyote ya Deschamps kufanya mabadiliko katika kikosi kilichoanza siku ya ufunguzi, lakini kiwango bora cha Payet kinaweza kumshawishi kufanya mabadiliko ya namba endapo Pogba hataonesha kiwango cha kuridhisha kwa mara nyingine leo.
Antoine Griezmann pia hakuwa katika ubora wake, lakini ni matarajio yangu kwamba ataanza katika nafasi yake dhidi ya kinda Kinsley Coman, huku Giroud pia akiendelea kubaki kama mtu wa mwisho kutokana na ubora wake anaoendelea kuonesha mbele ya lango.
Albania kwa upande wao, wanaingia katika mchezo wa leo wakiwa na kumbukumbu ya kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Uswizi na bado wanabaki na matumaini ya kusonga mbele endapo tu watashinda mchezo wa leo.
Licha ya kucheza pungufu kwa takriban dakika 54 baada ya nahodha wao Loric Cana kutolewa nje kwa kadi nyekundu, lakini Albania walionesha kiwango cha hali juu sana. Walikuwa na bahati mbaya kutopata bao la kusawazisha katika dakika za mwisho baada ya kipa wa Uswizi kufanya kazi ya ziada kuokoa hatari nyingi ambazo zingeleta madhara makubwa.
Lakini katika mchezo wa leo, Ufaransa wanapewa nafasi kubwa zaidi, lakini hofu yao kubwa inakuja kutokana na kutokuwa na rekodi nzuri dhidi ya wapinzani wao katika michezo miwili iliyopita.
Takwimu za mechi zao walizokutana.
- Ufaransa wameshinda michezo minne kati ya sita waliyocheza dhidi ya Albania lakini wameshindwa kupata matokeo katika michezo miwili ya mwisho.
- Goli la Mpira wa adhabu wa uliopigwa na Ergys Kace liliipa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ufaransa katika mchezo uliofanyika June 2015.
- Albania hawajawahi kufunga goli zaidi ya moja kwenye mchezo dhidi ya Ufaransa (wamefunga magoli 3 katika michezo sita).
- Ufaransa katika jumla ya ya michezo 13 waliyocheza katika jiji la Marseille, wamepata matokeo haya (Ushindi mara sita, sare mara 3 na kufungwa mara 4).
- Wameshawahi kucheza katika uwanja huu mara mbili kwenye mashindano haya. Walifungwa 2-0 na Czechoslovakia mwaka 1960, lakini wakaibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Ureno mwaka 1984.
- Ufaransa wameshinda mechi zao sita za mwisho katika ardhi yao ya nyumbani kwenye michuano ya Ulaya (tano wakishinda mwaka1984 na moja mwaka 2016).
- Ufaransa wamepata ‘clean sheets’ mbili tu katika michezo yao 17 ya mwisho kwenye michuano ya Ulaya (dhidi ya Romania mwaka 2008 na Ukraine mwaka 2012).
- Katika michezo sita ya mwisho aliyoanza akiwa Ufaransa, Olivier Giroud amefunga nane.
- Mashuti matano ya Ufaransa yaliyolenga lango (ukijumlisha na yale yaliyozaa magoli katika mchezo wa ufunguzi) dhidi ya Romania yote yamepatikana katika kipindi cha pili.
- Dimitri Payet alitengenea nafasi nane katika mchezo dhidi ya Romani. Ni wachezaji watatu tu waliofanya zaidi yake tangu mwaka 1980 (Ozil, 9 vs Ugiriki mwaka 2012, McAllister, 10 vs Ujerumani mwaka 1992 na Sneijder, 10 vs Denmark mwaka 2012)
- Albania wamepoteza michezo yao miwili ya mwisho. Hawajawahi kupoteza michezo mitatu mfululizo tangu Oktoba mwaka 2013.
- Wanaungana na Iceland kuwa mataifa mawili kucheza kwa mara ya kwanza mashindano ya Euro mwaka huu 2016.
- Albania wanakuwa ni taifa la nne kwa mchezaji wake kupewa kadi nyekundu wakati wakishiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza (England mwaka 1968, Uholanza mwaka 1976 na Bulagaria mwaka 1996).
- Etrit Berisha akliokoa michomo minne katika mchezo dhidi ya Uswizi, mara nyingi zaidi ya aliyookoa wakati wa michezo ya hatua ya kufuzu kucheza mashindano haya.
Didier Deschamps, Ufaransa: Tunapaswa kushinda mchezo wa leo, hata ikitokea mchezo unakuwa mgumu kama wa awali lazima tuwe na uvumilivu. Albania ni timu nzuri, wana kocha kutoka Italy. Wako vizuri sana hasa kwenye matumizi ya nguvu lakini vile vile akili. Katika mchezo wa kirafiki tuliocheza nao mwaka jana, walitupa wakati mgumu sana pengine kwa sababu wachezaji wengi walikuwa mapumzikoni..lakini yote kwa yote ni ni timu nzuri.”
Gianni De Biasi, Albania: “Tulicheza vyema dhidi ya Uswizi, tumefika langoni mwao mara tatu, tulitengeneza nafasi nyingi sana. Takwimu zinaonesh kwamba lazima tutapata goli katika mchezo wa leo…ukiangalia kwenye suala la ubora, Ufaransa ni moja ya mataifa bora duniani, na uwepo wao katika ardhi ya nyumbani ni faida nyingine kwao..wanapewa nafasi kubwa sana ya kushinda mchezo huu kuliko sisi, lakini naahidi kusimama imara na kuhakikisha tunapata matokeoa licha ya kuwa wametuacha mbali katika viwango vya FIFA (FIFA ranking).
No comments:
Post a Comment