Tuesday, 23 February 2016

Askofu ashauri halmashauri kuajiri walioelimika

ASKOFU wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga, Mhashamu John Ndimbo ameishauri Halmashauri ya Mji wa Mbinga kuajiri watumishi walioelimika vya kutosha ili kuongeza kasi ya maendeleo endelevu ya halmashauri na wilaya kwa ujumla.
Askofu Ndimbo alisema hayo jana katika kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo, na kuongeza kuwa kuajiri watumishi maamuma ni kupinga falsafa ya Serikali ya Awamu ya Tano inayokazia juhudi katika kuharakisha maendeleo katika jamii.
Ndimbo ambaye alialikwa katika mkutano huo akiwawakilisha viongozi wa dini ya Kikristo, aliongeza kuwa kwa uzoefu wake hakuna mahali popote panapoweza kuendelea ikiwa elimu itaachwa nyuma.
“Awe ni Ofisa Mtendaji au Mtendaji wa Kijiji, ni vigumu sana na itakuwa ndoto kama tutamtarajia asimamie miradi ya maendeleo kama yeye mwenyewe hajitambui na hana ujuzi na weledi,” alisema.
Alifafanua kuwa ikiwa halmashauri hiyo inatamani kuona wakuu mbalimbali wa Idara wanabaki katika nafasi zao bila kuhamishwa au kusimamishwa kazi, hakuna njia ya mkato zaidi ya kuhakikisha kuwa watumishi hao wanajiendeleza kielimu mpaka watimize vigezo vinavyotakiwa na mwajiri.
Akitoa mfano hai, Askofu huyo alisema hivi karibuni katika vyombo vya habari aliwanukuu wakubwa serikalini waliutaja mkoa wa Ruvuma miongoni mwa mikoa iliyofanya vizuri katika suala la mapambano dhidi ya kipindupindu na usafi wa mazingira lakini akawataka wasijisahau.

No comments:

Post a Comment