Monday, 18 January 2016

Niyonzima aiomba radhi klabu ya Yanga

Mchezaji wa Timu ya taifa ya Rwanda na klabu ya Yanga Haruna Niyonzima hatimaye ameiomba radhi klabu hiyo kutokana na matatizo yaliyojitokeza baina ya mchezaji huyo na klabu yake.Nyota huyo wa kimataifa wa Rwanda alikuwa katika mgogoro na klabu hiyo hatua ambayo imepelekea kuondolewa katika kikosi cha timu hiyo kwa madai ya utovu wa nidhamu.
Niyonzima ameomba radhi kwa yote yaliyotokea na kuwataka viongozi wake kufikiria upya suala lake,ambapo awali ilitolewa taarifa ya kutimuliwa na kudaiwa kulipa fidia ya mamilioni ya fedha na klabu hiyo.
Kwa mujibu wa uongozi wa Klabu ya Yanga, wameyapokea maombi hayo ya Niyonzima, na uongozi wa klabu hiyo utakutana ili kuona jinsi ya kulitatua tatizo la kiungo huyo.
Wakati huo huo klabu ya yanga imefanikiwa kurejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ndanda FC katika mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Bao hilo pekee limefungwa na Kevin Patrick Yondan kwa mkwaju wa penalti na kufikisha alama 36 baada ya kucheza mechi 14, ikilingana na Azam FC iliyopo nafasi ya pili.

No comments:

Post a Comment